Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Lindi

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, amewataka wananchi kuwachagua viongozi wa chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za kijamii katika vijiji na vitongoji.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kitongoji cha Madiga, Kijiji cha Darajani, Kata ya Kipatimu, Jimbo la Kilwa Kaskazini, Mkoa wa Lindi, Alhamisi Novemba 21, 2024, Semu amewahakikishia wananchi kuwa ACT Wazalendo imejipanga kulinda kura zao ili kurejesha nguvu ya wananchi na kusukuma maendeleo.

“Mwenyekiti yeyote wa ACT Wazalendo atakayeshindwa kutimiza majukumu yake, tutamwajibisha kabla ya wananchi kufanya hivyo,” amesisitiza Semu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi wa Baraza Kivuli la ACT Wazalendo, Idrisa Kweweta, amewataka wananchi kutumia uchaguzi huu kuonesha hasira zao dhidi ya CCM kwa kile alichokitaja kuwa ni “hujuma za dola zinazodumisha hali duni ya maisha vijijini.”

“Katika Jimbo zima la Kilwa Kaskazini, CCM imebaki na wagombea tisa tu kati ya 34 wa vijiji. Nyinyi mliobaki lazima mtume ujumbe kwa kuchagua viongozi wa ACT Wazalendo waliobaki ili kuonesha kuwa CCM haitakiwi,” amesema Kweweta.

Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Kijiji cha Darajani, Marunga Said Kilindo, ameahidi kuwa atarejesha mradi wa maji, kuongeza vyumba vya madarasa, na kuchonga barabara ili zifae kwa matumizi ya muda wote. Pia amesema atashirikiana na wananchi katika kuleta maendeleo ya kijiji hicho.