Na Mwandishi wetu, JamhuriMedia
Chama cha ACT Wazalendo kimesema hakikubaliani na matokeo ya ubunge yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kutangazwa jana na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbarali Missana Kwangura .
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo,Ado Shaibu akizungumza baada ya matokeo hayo kutangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mbarali ambapo alimtangaza, Bahati Keneth Ndingo kwa kura 44334 dhidi ya kura 10014 za Modestus Kirufi wa ACT Wazalendo.
“Uchaguzi ulikuwa na kasoro nyingi sana,ikiwemo Msimamizi wa Uchaguzi alivuruga sana zoezi la kuapisha mawakala. Maeneo ambayo aliahidi kuja kuapisha mchana alifika usiku hiyo ilisababisha baadhi ya mawakala wetu na wa vyama vingine wasiapishwe,”amesema na kuongeza
“Cha kustaajabisha, asubuhi ya siku ya kupiga kura, CCM ilikuwa na mawakala katika vituo vyote,CCM ilitumia vituo ambavyo mawakala wetu walizuiwa, kuweka matokeo ya uongo. Ni jambo la kustaajabisha eneo lenye vyumba vitatu, vyumba vyenye mawakala vina mahudhurio hafifu lakini chumba ambacho hakina mawakala kinapewa mahudhurio ya asilimia 100 au zaidi” amesema.
Aidha amesema maombi yao ya kutaka vituo vyote vyenye utata masunduku yake yahesabiwe upya yalipingwa na Msimamizi wa Uchaguzi.
Katika hatua nyingine, Ado amesema kuwa kasoro zinazojitokeza kwenye chaguzi za marudio zinaitia doa Serikali ya Awamu ya Sita hasa katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.
Amesema kuwa Chama cha ACT Wazalendo kitafanya uchambuzi wa kina wa kasoro zilizojitokeza kwenye Chaguzi zote za marudio na kuandaa Ripoti Maalum itayowasilishwa kwa wadau ikiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa.
Naye Mgombea wa Ubunge Modestus Dickson Kirufi amesema uchaguzi umekuwa na kasoro nyingi na ni muhimu mamlaka zinazohusika ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi zifanyie kazi kasoro hizo. Pia amesema anasikiliza msimamo wa Chama kujua hatua inayofuata baada ya matokeo kutangazwa.