Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar
Msemaji wa Sekta ya Katiba na Sheria ya ACT-Wazalendo, Victor Kweka kuwa amemshauri Rais Samia Suluhu Hassan kuunda tume ya majaji ili kupitia malalamiko ya wananchi waliolipishwa fedha kwa kukiri makosa na kulipa fedha serikalini.
Hatua hiyo inatokana na kuibuka tena kwa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),Charles Kichere zinazohusu kuendelea na uchunguzi wa akaunti ya fedha zilizokusanywa kutokana na utaratibu wa makubaliano ya kukiri kosa ‘plea bargaining’ na ripoti yake kutarajiwa kutolewa mwezi Machi 2023. Kauli hii imechochea mjadala na kuzalisha mapendekezo tofauti tofauti kutoka kwa wadau mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa msemaji huo amesema kuwa mnamo mwaka wa 2019, Bunge lilitunga Sheria ya makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining) ambayo iliweka utaratibu wa makubaliano maalumu katika kesi ya jinai kati ya Mwendesha Mashtaka na Mshitakiwa. Kupitia utaratibu huu mshitakiwa anakubali kosa moja au zadi katika makosa aliyoshitakiwa nayo ilia pate nafuu ya kesi hiyo.
Amesema kuwa itakumbukwa kuanzia mwaka 2017 lilizuka wimbi la Serikali kushiriki uporaji dhidi ya mali za watu, wakiwemo wawekezaji kupitia kesi za kubambikiwa za Uhujumu Uchumi. Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka – DPP ilianza kutaifisha fedha za watu bila ya kuwepo kwa Sheria ya ‘plea bargain’. Baada ya malalamiko ndipo sheria ikatungwa. Kwa muda wa miaka 4 tumeshuhudia watu wengi wakiporwa mali zao ili kupata uhuru wao.
Katika uchambuzi wetu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesbabu za Serikali (CAG) mwaka jana (2021) tulisema kuwa CAG amekuta kuna fedha kiasi cha Shilingi bilioni 51.521 kutokana na kesi zilizomalizika katika Mahakama mbalimbali kwa kipindi cha miaka 6. Kwa mujibu wa CAG fedha hizi hazikutumika kwa sababu ya kukosekana kwa sheria na kanuni za matumizi yake.
Amesema kuwa wakati Watanzania wakisubiri ripoti ya ukaguzi wa fedha na utaratibu wa kesi zilizohitimishwa kwa kufuata sheria ya makubaliano ya kukiri kosa, ili kujiridhisha na taratibu zote na kubaini kiasi halisi kilichokusanywa kutokana na utaratibu huo chama kimependekeza Jaji Biswalo Mganga kujiuzulu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na pia Jaji Kiongozi kutompangie kazi Jaji Biswalo hadi uchunguzi utakapokamilika na kujua hatma ya maamuzi ya uchunguzi wa fedha za Plea bargaining.
Pia imependekeza kuwa watakaobainika walilazimishwa kukiri makosa warejeshewe fedha zao zote.