ACT Wazalendo imeguswa na uamuzi wa Serikali ya Marekani kusitisha kwa muda kwa mikopo na ruzuku za kusaidia huduma za afya Duniani, hatua inayoweza kuathiri mamilioni ya Watanzania waliowekwa kwenye utegemezi wa huduma za afya zinazofadhiliwa na mashirika ya nje.
Tanzania, kama moja ya wanufaika wakubwa wa misaada ya hiyo kutoka Marekani kupitia Shirika la Misaada ya Marekani (USAID), Mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI (PEPFAR), Mfuko wa Dunia (Global Fund), Mpango wa Kupambana na Malaria (PMI) imechangia kwa kiasi kikubwa katika mapambano dhidi ya magonjwa kama UKIMWI, kifua kikuu, malaria, na huduma za chanjo kwa watoto.
Kwa Mfano, hadi kufikia Machi 2024, Tanzania ilikadiriwa kuwa na watu milioni 1.7 wanaoishi na VVU, ambapo zaidi ya milioni 1.5 wanatumia dawa za kufubaza makali ya UKIMWI (ARVs) tunazotegemea kutoka nje.
Mapema mwaka huu Global Fund ilitangaza ufadhili wa dola za Marekani milioni 602. Sawa na Shilingi trilioni 1.57 kwa matibabu endelevu ya waathirika wa VVU.
Aidha, ACT Wazalendo kupitia Baraza Kivuli la Mawaziri tumekuwa tukiionya Serikali kuhusu utegemezi huu wa kifedha kutoka nje kwenye kutoa huduma za afya, ambapo unaweka rehana maisha ya watanzania. Takriban 41% ya bajeti ya afya ya Tanzania inategemea Mashirika ya misaada ya kimataifa, tena kwa huduma za magonjwa hatari zaidi.
Kwa miongo mitatu, Serikali ya CCM imekuwa ikiacha suala la afya kwenye mabega ya wananchi wenyewe au wafadhili kutoka nje. Bajeti ya afya ya Tanzania ni chini ya asilimia 5 ya bajeti kuu ya Serikali, kinyume na makubaliano ya Abuja yanayotaka kutengwa kwa asilimia 15 ya bajeti kuu kwa ajili ya sekta ya afya.
Hivyo, uamuzi huu utaivua nguo Serikali kwa kuweka wazi makosa yake ya kutoweka kipaumbele kwa afya na kuweka maisha ya Watanzania kwenye mikono ya wafadhili wa kigeni.
ACT Wazalendo, hatutaki makosa ya Serikali ya CCM yasiwaangamize watanzania, tunaitaka Serikali ichukue hatua zifuatazo;
Serikali ipunguze matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha kwenye huduma za afya zinazotishiwa na kusitishwa kwa misaada ya nje.
Kuanzisha Mfuko wa Huduma za Afya ya Kitaifa kwa kutumia rasilimali za ndani kama madini na utalii kufadhili mfumo wa afya unaojitegemea.
Serikali iongeze bajeti ya afya kutoka wastani wa asilimia 5.7 hadi kufikia 10% ya bajeti kuu 2025/2026, ili kupunguza utegemezi na kuboresha huduma ya afya.
Serikali iharakishe utekelezaji wa mfumo wa kuwaunganisha watanzania na Hifadhi ya Jamii na kutoa bima ya afya kwa wote ili kuongeza uwezo wa serikali kugharamia na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila ubaguzi wa kifedha.
ACT Wazalendo tunasisitiza kuwa ni wajibu wa Serikali ni kuhakikisha inatumia rasilimali vizuri ili kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wote kwa usawa, si kwa kutegemea wafadhili wa nje. Serikali haipaswi kufanya mambo ya anasa huku ikiwaacha wanachi wake wanaishi kwa kutegemea hisani.
Dkt. Elizabeth Benedict Sanga
Waziri Kivuli wa Afya
ACT Wazalendo
29 Januari, 2024