Chama cha ACT Wazalendo kimetoa msimamo wa kuunga mkono na kuongoza mapambano ya wananchi katika kukabiliana na wimbi kubwa la uporaji wa ardhi nchini. Viongozi wa chama wamesikitishwa kukutana na kero ya migogoro, uporaji na operesheni za Serikali kuwaondoa wananchi kwenye ardhi yao kila jimbo walilopita kwenye ziara ya Chama inayoendelea. Vitendo hivi vinaondoa usalama na uhakika wa milki ya ardhi kwa wananchi na kudhoofisha maendeleo yao, na ni lazima vikomeshwe.

Msimamo huo umetolewa na viongozi wakuu wa ACT Wazalendo wakiendelea na ziara ya awamu ya kwanza ya kuyafikia majimbo 214 ya Tanzania Bara wakiwa kwenye majimbo ya Bunda Vijijini (Mara), Mbulu (Manyara), Newala Mjini (Mtwara) na Kigoma Kusini (Kigoma).

Akiwa Mbulu Manyara Kiongozi wa Chama Dorothy Semu amesema ACT Wazalendo inapata wasiwasi kukikithiri kwa malalamiko ya wananchi kwenye ardhi na kwamba hatua zinazochukuliwa na Serikali hazisaidii kulinda haki za wananchi hao.

“Migogoro ya ardhi nchi kwetu inazidi kuongezeka, wafugaji na wakulima, wananchi dhidi ya Serikali, wananchi dhidi ya wawekezaji kwa nyakati zote waathirika ni wananchi, wao ndio wanapoteza haki zao za kutumia ardhi. Mara kadhaa tunashuhudia mauaji, mapigano, kufukuzwa au uhamishaji wa wananchi kwenye ardhi zao.” Amesema Ndg. Semu.

Ameeleza kuwa, kiini cha matatizo yote wanayopitia wananchi kwenye ardhi ni ardhi kuwekwa kwenye mikono ya Rais, hivyo Serikali kujipa mamlaka ya mwisho katika kutwaa, kudhibiti na kumiliki ardhi bila ridhaa ya wananchi.

“Nataka niwaambie mfumo huu unamfanya Rais kuichezea ardhi kwa utashi wake, akipata mteja wa kufuga wanyama sehemu yoyote ya ardhi nchini anaweza kuwaondoa watu kwenye ardhi hiyo ili tu kumpisha huyo mtu afuge, hii ndio maana ya yote tunayoyaona.’’ Amesema Ndg. Semu.

Naye, Makamu Mwenyekiti Isihaka Mchinjita amesema kasi ya kupandisha hadhi na kupanuliwa kwa maeneo ya hifadhi imeongeza migogoro. Wananchi wanaoishi karibu na maeneo hayo wameishia kuporwa ardhi, kupitia ukandamizaji, udhalilishaji na mateso makubwa.

“Serikali imekuwa ikipanua maeneo ya hifadhi kwa kumega ardhi za wananchi kwa kutumia nguvu kubwa. Wakati tunapata uhuru eneo lote la hifadhi lilikuwa sawa na 12% ya ardhi yote huku tukiwa na idadi ndogo ya watu. Kwa sasa eneo la hifadhi linachukua 38 ya ardhi yote na sasa tunasikia tetesi kwamba Serikali inataka kuongeza eneo la hifadhi kufikia 50% ya ardhi.” Amesema Ndg. Mchinjita.

Amesisitiza kuwa Serikali ya CCM inajali zaidi wanyama na wawekezaji kwakuwa inachukulia ardhi inapaswa kutengeneza faida zaidi kuliko kukidhi mahitaji ya kijamii. Ndio maana inapora ardhi kutoka kwa wananchi wazawa na kuanzisha ‘hifadhi’ kwa ajili ya wawekezaji.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ndg. Ado Shaibu ameeleza mfumo na sheria ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kuwa na mapungufu yanayotishia haki na usalama wa ardhi za wananchi vijijini. Amesema mfumo uliopo wa mabaraza hauna utaratibu wa uwajibikaji kwakuwa unasimamiwa na mamlaka zaidi ya moja. Ametaja mapungufu mingine ya kiuendeshaji kama vile uelewa mdogo wa wajumbe katika mabaraza ya vijiji na kata, rushwa na upendeleo.

“Nchi yetu kuna ardhi ya kijiji na ardhi ya jumla, wananchi vijijini wanapoteza ardhi kutokana na viongozi wabovu wa vijiji. Wengi wao ni wala rushwa, wababe na hawawashiriki wananchi. Wanapora mamlaka ya Mkutano wa Kijiji kwenye kuamua masuala ya ardhi kama sheria inavyotaka”. Amesema Ndugu Ado.

Naye Kiongozi Mstaafu wa Chama Ndg. Zitto Kabwe akiwa Ilagala Kigoma Kusini (Kigoma) alieleza kuwa anaona kila dalili ya kutokea vita nchini itakayohusisha ardhi; na hususani vita hiyo itakuwa kati ya kundi la wakulima na wafugaji.

Akieleza sababu kubwa ya hofu yake amesema malalamiko juu ya migogoro ya ardhi yamekuwa makubwa na yanazidi kuongezeka badala ya kupungua.

‘’Nchi yetu hii, sioni pakiwa na vita kati ya dini; sioni pakiwa na vita ya kikabila. Lakini kwa hali ninavyoiona ya mienendo ya migogoro ya ardhi; migogoro kati ya wakulima na wafugaji, naogopa sana kwamba tishio la amani katika nchi hii litahusu ardhi. Kwa sababu malalamiko ya watu kuhusu ardhi ni makubwa sana.’’ Alisema Ndugu Zitto.

Ndugu Zitto ameitupia lawama serikali ya CCM kwa kushindwa kushughulikia tatizo hilo, akisema kuwa CCM imechoka na haina mbinu mpya ya kushughulika na matatizo ya watanzania.

Imetolewa na;

Shangwe Ayo
Naibu Katibu Idara ya Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma
ACT Wazalendo
30 Julai, 2024

Please follow and like us:
Pin Share