Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Chama cha ACT Wazalendo kimezindua Sera ya jinsia ikiwa ni mwelekeo na jitihada za chama hicho kuongeza ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi.

ACT Wazalendo kimekuwa chama cha kwanza cha siasa kuwa na sera ya jinsia nchini.

Akizidua sera hiyo, leo katika mkutano mkuu wa Ngome ya Wanawake wa ACT Wazalendo leo Machi 2, 2024 mwanaharakati wa masuala ya jinsia na haki za binadamu, Dk Ananilea Nkya amesema sera hiyo ya jinsia itakiweka chama hicho kwenye nafasi nzuri ya ushiriki wa wanawake katika siasa.

Nkya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (JUKATA) amesema tatizo kubwa la kudumaa kwa maendeleo nchini ni kutokana na wanawake wenye uwezo kutoshiriki michakato ya kisiasa wakihofia mifumo dume.

“Nchi yetu inashindwa kupiga hatua za maendeleo kutokana wanawake na wanaume wenye uwezo wa kuongoza kuhofia mifumo iliyopo ambayo inafanya watu wenye uwezo wasichagulike kutokana na Katiba mbovu iliyopo sasa.

“Niwaombe wanawake mliopo hapa hiyo sera ya jinsia iliyozinduliwa leo iwe nyenzo muhimu ya kuandaa wanawake shupavu huko vijijini wagombee nafasi kuanzia serikali za mitaa ili kupigania haki za Watanzania.” amesema Nkya.

Akizungumzia umuhimu wa sera hiyo, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Tanzania Bara, Doroth Semu amesema ushiriki wanawake kwenye nafasi za maamuzi ndani ya chama hicho bado ni mdogo ukilinganishwa na wanaume.


Amesema hali hiyo inatokana na kuwapo ombwe kubwa linalochangiwa na uwepo wa mifumo kandamizi isiyolenga kumpa mwanamke nafasi kwenye ngazi za maamuzi.

“Ndani ya chama kwa ngazi ya sekretarieti uwiano wa idadi ya wanawake ni asilimia 34.6, ngazi ya kamati kuu idadi ya wanawake ni asilimia 35 3, halmashauri kuu ni asilimia 28.4 na mkutano mkuu ni asilimia 11.4 amesema.