Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kupeleka bungeni muswada wa marekebisho ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuvifanyia mageuzi makubwa vyombo vya haki jinai na mfumo wa uchaguzi kwa ujumla wake.
Akizungumza leo katika makao makuu ya chama hicho, Magomeni Dar es Salaam, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita amesema hatua hiyo imetokana na kutokuwa na imani juu ya usimamizi wa uchaguzi wa marudio wa udiwani uliofanyika kwenye kata 23 Machi 20, 2024.
“Chama cha ACT Wazalendo kilisimamisha wagombea sita, Chipuputa, Wilaya ya Nanyumbu, Kabwe, Wilaya ya Nkasi, Kasingirima Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mlanzi Wilaya ya Kibiti, Kamwene, Wilaya ya Mlimba na Bukundi Wilaya ya Meatu,” amesema Mchinjita.
Mchinjita amesema utaratibu wa uhifadhi na usambazaji wa karatasi za kupigia kura unahitaji kuangaliwa upya ikiwemo kushirikisha vyama vya siasa na wadau wengine kwenye kila hatua.