Na Magrethy Katengu,JamuhuriMedia
Dar es Salaam
Wakati Daftari la Kudumu la Kujiandikisha la Kupiga kura zoezi likianza Oktoba 11, 2024 Chama cha ACT – Wazalendo kimesema kuna baadhi ya mambo hayako sawa hivyo wameiomba TAMISEMI kuwa na uwazi, uadilifu na mfumo maalum wa utoaji wa taarifa zinazohusu uchaguzi huu kwa kuvishirikisha vyama katika ngazi ya taifa ili visaidie kutoa ufafanuzi kwa viongozi wao wa ngazi za chini.
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 10,2024 Jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa ACT -Wazalendo, Ado Shaibu, amesema hakuna mtiririko juu ya utoaji wa taarifa na maelekezo kuhusu utaratibu mzima wa uchaguzi, kila ngazi na kila eneo Wasimamizi wa Uchaguzi huu wanatoa taarifa wajuavyo wao na kwa muda wanaoupanga wao.
“Pamoja na kwamba TAMISEMI wametoa Kanuni na Mwongozo kuhusu mchakato mzima wa Uchaguzi lakini katika zoezi la Vyama vya Siasa kutoa Mawakala wa Uandikishaji wa Wapiga kura imeishia kuelezwa kuwa ni haki ya vyama kupeleka Mawakala kuapa tarehe zimekuwa zikileta mkanganyiko baadhi ya maeneo ikiwemo Newala ”amesema Ado.
Ameongeza kuwa kuelekea siku ya kupiga Kura ili kuondosha sintofahamu zilizojitokeza wakati wa maandalizi ya kuandikisha wapiga kura, TAMISEMI inapaswa kueleza ni lini Majina ya Mawakala yanapaswa yawe yamewasilishwa kwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi na tarehe iwekwe wazi wataapishwa ili kuvipa vyama nafasi ya kujiandaa.
“Kwa Mujibu wa kanuni ya Uchaguzi na Kalenda ya Matukio, TAMISEMI wameonesha kuwa Fomu ya kuaomba kuteuliwa kuwa mgombea itachukuliwa siku zisizopungua ishirini na sita kabla ya siku ya Uchaguzi Kif. 17 (1) na kutakiwa kuzirejesha ndani ya siku saba Kif. 17 (2). Hii maana yake Fomu ya uteuzi itatolewa kwa siku moja tu yaani tarehe 1 Novemba, 2024 isipokuwa unaweza kurejesha wakati wowote ndani siku saba (tarehe 1 mpaka 7), wameshindwa kuzingatia kuwa upo uwezekano wa mgombea kuumwa au kupata tatizo litakalopelekea yeye kushindwa kwenda kuchukua Fomu siku hiyo”amesisitiza Ado.
Hata hivyo amesema TAMISEMI imeombwa kuweka utaratibu rafiki wa vituo vya kuapishia Mawakala badala ya kuwataka Mawakala hao wasafiri kwa umbali mrefu kufuata kuapishwa wakati hali halisi kinachofanyika kwenda kujaza Fomu za kiapo jambo ambalo linaweza kufanyika mahala popote karibu yao bila kuathiri maana na mantiki ya kiapo hicho.
Sambamba na hayo amesema ACT -Wazalendo watashiriki Uchaguzi wakipambana hivyo wamewasihi wananchi kujitokeze kwa wingi kwenda kujiandikisha katika daftari la kudumu la.
Wakazi wa Mtaa ili watumie haki yao vizuri katika Uchaguzi huu kuwachagua wawakilishi wanaowaona kuwa wataweza kusimamia maendeleo ya maeneo yao.