Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbeya

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, ameongoza kampeni za chama hicho Ijumaa, Novemba 22, 2024, akimnadi mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa kijiji cha Warumba, Abdulkarim Abbas, katika Kata ya Songwe, Jimbo la Mbarali, mkoani Mbeya.

Ado Shaibu amesisitiza dhamira ya chama hicho ya kujenga usawa kwa wananchi wote. Akizungumza katika mkutano huo, alisema:

“Ukiangalia gari nililokuja nalo limeandikwa ‘Taifa la Wote Masilahi ya Wote.’ ACT Wazalendo, ahadi yetu kwa Watanzania mkituchagua, tutakachopigania ni taifa la wote kwa masilahi ya wote. Na katika uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa, kauli mbiu yetu ni hiyohiyo, vijiji vya wote, mitaa ya wote kwa masilahi ya wote.”

Shaibu ameongeza kuwa sera hizo ni tofauti na zile za Chama Cha Mapinduzi (CCM), akidai kuwa CCM haina sera zinazojumuisha wananchi wote:

“CCM yenyewe wanaimba mpaka nyimbo wanasema CCM ina wenyewe. Wewe Abdulkarim (mgombea uenyekiti wa ACT), ukipata nafasi, tutakushika mkono na kukusimamia mpaka ushinde. Sera yetu iwe Warumba ya wote kwa masilahi ya wote.”

Kwa upande wake, mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa kijiji cha Warumba, Abdulkarim Abbas, aMEwaomba wananchi wa kijiji hicho kumpa nafasi ya uongozi ili aweze kushughulikia changamoto zinazowakabili, hususan tatizo la maji.

“Ninaomba mnipe kura zenu. Shida zinazowapaga watu wa Warumba ni shida ambazo zinanipata na mimi, kwa sababu ninaishi katika kijiji hiki. Kuna suala la ukosefu wa maji; kina mama wengine mpaka saa 12 asubuhi wanafuata maji. Haya si matatizo ya Mwenyezi Mungu, bali ni matokeo ya viongozi wasiowajali wananchi, wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi.”

Abdulkarim amesisitiza kuwa ni wakati wa wananchi wa Warumba kufanya mabadiliko kupitia uchaguzi huu:

“Katiba imeruhusu kila baada ya miaka mitano watu wafanye masahihisho. Niwaombe wenzangu Wanawarumba tufanye masahihisho. Yapo mengi ambayo nimekusudia kuyafanya.”