Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo Taifa, Abdul Nondo, amewataka wananchi wa Kijiji cha Kizenga, Kata ya Bitale, Jimbo la Kigoma Kaskazini, kuchagua wagombea wa ACT Wazalendo katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, ili kurejesha mamlaka yao ambayo amedai kuwa yamehodhiwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Novemba 25, 2024, kijijini Kizenga, Nondo amesema kuwa uongozi wa CCM umeshindwa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa kijiji hicho, hali ambayo imesababisha baadhi yao kukata tamaa ya kushiriki katika masuala ya uchaguzi.

Amesema wananchi wa Kizenga wanapaswa kutumia fursa ya uchaguzi huu kurejesha mamlaka yao kwa kuchagua wagombea wa ACT Wazalendo ambao wanadhamiria kuleta mabadiliko ya kweli.

Nondo ametaja changamoto zinazoikabili jamii ya Kizenga, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa jengo la mama na mtoto, michango holela isiyo na uwazi, upendeleo katika utoaji wa msaada wa TASAF, na changamoto katika sekta ya elimu.

Amesema changamoto hizi zimekuwa mzigo mkubwa kwa wananchi, huku akisisitiza kuwa ACT ina mpango wa kushughulikia changamoto hizo kwa kuwashirikisha wananchi moja kwa moja.

Amewahimiza wananchi wa kijiji hicho kuacha kusikiliza propaganda zinazolenga kuwakatisha tamaa na badala yake kuamini kuwa sauti yao kupitia kura ndiyo njia ya kuleta mabadiliko ya kweli katika kijiji hicho na maeneo mengine.