Yatoa mpango wa kufufua maendeleo Nambani, Dar

Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Mtaa wa Mtambani kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Mohammed Mtutuma, ametoa ahadi ya kupambana na unyanyasaji na kuhakikisha heshima ya wananchi inalindwa, ikiwa ni sehemu ya kampeni zake kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Akizungumza mbele ya wananchi wa mtaa huo uliopo Kata ya Vingunguti, Jimbo la Segerea, Dar es Salaam, Novemba 25, 2024, Mtutuma amesema:

“Serikali ya ACT Wazalendo chini ya Mohammed Mtutuma, hatutakubali watu wadhalilishwe kwa kupigwa bakora kwenye mtaa huu wa Mtambani. Lazima tulinde heshima yao, utu wao ni muhimu kuliko madaraka yetu. ACT chini yangu na viongozi wengine tutaanzisha mchakato wa kufufua visima ambavyo aliyekuwa anatawala mtaa huu na wenzake wameviharibu.”

Mtutuma ameongeza kuwa chama chake kinaamini katika uwajibikaji na uadilifu, akitoa mfano wa ufisadi uliobainika kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022/2023, katika kata ya Vingunguti.

“Taarifa ya CAG inasema wazi, kata ya Vingunguti kumeundwa vikundi 34 hewa na fedha zake zimewekwa mifukoni. Vikundi hivyo vinaanzia serikali ya mtaa. Ni nani aliunda na kusaini fomu ya vikundi hewa kwenye Mtaa wa Mtambani? Leo wanakuja kutuambia wanataka kuijenga Mtambani mpya. Ya zamani aliibomoa nani?”

Katika mkutano huo, Mwenyekiti mstaafu wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji, maarufu kama Babu Duni, alimnadi Mtutuma kwa wananchi wa Mtambani, akiwataka kumchagua kwani ni kiongozi anayeweza kutatua changamoto zao.

“Sasa tarehe 27 Novemba, nafsi yako ndiyo itakayokuambia nimpigie fulani au huyu Mtutuma. Shida za Mtambani mnazipata nyinyi, mateso ya Mtambani mnayajua nyinyi. Ninaapa kwa dini yangu, uamuzi wako wa kumpigia mtu fulani ni wako, lakini hakikisheni mnafanya uamuzi sahihi.” Amesema Babu Duni.