Wiki iliyopita kulitokea sintofahamu kati ya dereva wa gari la Gazeti la JAMHURI na mmoja wa matrafiki. Baada ya tukio hilo nilibaini chembe chembe za uonevu na nikaamua kuchukua hatua za kisheria kupitia mkondo wa utawala dhidi ya askari aliyekamata gari hilo. Jeshi la polisi lilisikiliza maelezo yetu na muda mfupi baada ya kutoka polisi niliandika kwenye mitandoa ya kijamii ujumbe ufuatao:-
Leo [Ijumaa Mei 28, 2017] nimefarijika sana baada ya Kamanda wa Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZTO), ACP Awadhi Haji kusimamia Sheria na kumwamuru askari wa Usalama Barabarani WP Beatrice alipe faini ilipobainika kuwa alitaka kumbikia kosa la kupita kwenye taa nyekundu Dereva wa Gazeti la JAMHURI.
WP Beatrice alilazimisha kuwa Dereva Leonce [William] Mujumuzi amepita taa nyekundu wakati alipita taa ya kijani baadaye akabadili kauli na kusema yeye alikuwa anaongoza magari hivyo Dereva Leonce hakupaswa kufuata ishara ya taa bali maelekezo yake WP Beatrice.
Katika kikao tulichofanya Ofisi ya ZTO Awadhi leo Aprili 28, 2017 Dar es Salaam, Afande Awadhi amesema amebaini ukweli kuwa WP Beatrice hakufuata utaratibu anaopaswa kufuata askari anapomkamata Dereva kwa kosa analomtuhumu nalo barabarani.
Nitaandika kwa kina sakata hili kwenye safu yangu ya SITANII Jumanne ijayo katika Gazeti la JAMHURI, ila kwa ufupi amesema askari akimkamata Dereva anapaswa kufanya yafuatayo:-
1. Askari akimkamata Dereva anaangalia aina ya kosa. Adhabu ya kwanza ni ONYO.
2. Adhabu ya pili imegawanyika sehemu mbili. Dereva akikiri kosa, anapigwa faini. Akikataa anapelekwa Mahakamani pande mbili zisikilizwe na haki itendeke.
Katika shauri lililokuwa mbele yetu, imethibitika WP Beatrice hakumpa fursa Dereva wetu Leonce ya ama onyo au kuchagua kati ya faini au kupelekwa mahakamani.
In charge wa Traffick Police Msimbazi Inspekta Bihemo, alikuwa ameelekeza Dereva Leonce awekwe ndani na kufunguliwa mashtaka kutokana na Leonce kulalamika kuwa WP Beatrice amemwonea.
ACP Awadhi amesema hayupo kutetea Polisi au Raia. Mwenye makosa anawajibika kwa makosa yake. Amebaini WP Beatrice amekiuka wajibu wake hivyo akamwagiza alipe faini aliyokuwa amemwandikia Leonce.
Nitaandika kwa kina kwenye safu yangu ila nampongeza ACP Awadhi. Sisi kama JAMHURI tumekuwa tukipokea malalamiko juu ya uonevu wa askari.
Si kwamba hatukuwa na Sh 30,000 za kulipa faini, ila tumejiuliza kama askari ana uwezo wa kutubambikia kesi sisi, inakuwaje kwa wasio na kuwasemea?
Ilitubidi tusimame kutetea haki. Tunamshukuru ACP Awadhi kwa kutetea na kusimamia haki bila uonevu.
Tunaamini WP Beatrice na Inspekta Bihemo kuanzia sasa watafanya kazi kwa weledi na kutenda haki kwa kila mmoja.
Asante ACP Awadhi na Mungu akubariki uendelee kusimamia haki, leo, kesho na baadaye.
Balile
 
Sitanii, baada ya kunadika waraka huu mfupi na kuuweka katika akaunti yangu ya facebook na mtandao wa Kijamii wa Jamiiforums, majibu yaliyokuja yamenishtua. Nimepata simu nyingi na simulizi zisizo kifani. Watu wanaeleza walivyoonewa hadi unasikitika.
Kwa kuwa tukio limekwishafahamika, nimeona badala ya kusimulia tena kilichotokea, bora kupitia safu hii niweke sehemu ya michango ya watu waliosoma andiko langu kwenye mitandao ya kijamii, polisi wapate fursa ya kusikia wananchi wanasemaje. Nimejaribu kuhariri sehemu chache ila maeneo ya msisitizo nimeyaacha yalivyo. Endelea…
Alex Fredric: Awadhi namfahamu sana ni mtu makini sana na ambaye anachukia rushwa sana.
Prosper Kamuzora Vedasto: Poleni sana, lakini ninyi ni moja ya alfu moja ya madereva tunaoamua kulipa faini kwa kuepuka usumbufu japo unaona kabisa UMEONEWA.
Nami nampongeza ACP Awadhi kama alivyowahi kufanya Kamanda mwingine (jina limenitoka) baada ya kulazimisha faini kwa dereva kuweka karatasi ya kiza, hali ni kwa ajili ya kuzuia jua kupiga usoni. Askari huyo alilazimika kulipa faini hiyo nadhani ilikuwa Oysterbay.
TATIZO ni askari wetu KUJIONA wapo juu ya sheria na kuhisi Watanzania hatujui HAKI zetu. Nadhani kuna UMUHIMU mkubwa katika gwaride la asubuhi kabla ya kupangiwa majukumu, askari wapewe “grill” ya ELIMU ya URAIA ili wafanye kazi kwa UADILIFU na WELEDI. Wanafanya wananchi tuichukie Serikali kwa kuhisi kuwa Traffic wamekuwa kitengo cha TRA!!!!!
HONGERA SANA ACP AWADHI.
Egbert Mkoko: Namfahami Afande Awadhi tangu alipokuwa Oysterbay Police. Ni mtu makini sana na huwa hamuonei wala kumpendelea mtu. Anafuata sana misingi ya kazi yake. Hata trafiki wenyewe husema wazi kuwa Awadhi ni mfano wa askari wa kuigwa kwa utendaji wake.
Hafidh Kido: Kamanda hili suala la kupita taa nyekundu wanalipenda sana, dah kumbe ndio mchezo waooo.
Swaleh Bafadhil: Mimi imenikuta leo [Jumamosi] tena tumesimamishwa gari mbili. Tuliweka msimamo kuwa hatuwezi lipa na kama kwenda mbele atupeleke.
Walipoona tumesimamia msimamo ikabidi waturudishie liseni zetu. Ila muhimu ni mtu kusimama na msimamo wako kwani huwa wanakuwa wengine kama kukujaribu.
John Monia: Tatizo sisi wengine ni vibarua inakuwa ngumu kukaa kwa huo muda mlokaa nyinyi.
Swaleh Bafadhil: Muda tuliokaa kaka ni dakika 8 tu.
Devis Leonard Mpandakyombo: Kweli askari baadhi yao huwa hawatutendei haki.
Kainerugaba Msemakweli: Kwa upande wa Beatrice, hii ndo maana [ya] zana (dhana) ya “Hapa Kazi Tu”.
Hanta Method: Pongezi tele kwa Kamanda Awadhi, ndo inavyotakiwa kufanya kazi kisomi sio kibabe!
Anastas Mbawala: Haya yalimkuta mfanyakazi mwenzangu, tena msichana alibambikiwa kesi na askari wa kike pale Mwenge, kuwa ametanua, lakini kumbe alitoka kumteremsha mfanyakazi mwenzake.
Askari alikataa kukubali na kusema huyo dada anamjibu kukataa na anaringa kwa vile ana gari. Akamsweka ndani hadi kesho yake [akapalekwa] mahakamani.
Ili asipoteze muda zaidi wa kazi alilazimika kukubali kosa, baada ya askari kubembelezwa sana [na] ndugu wa huyu dada na akabadilisha kosa kutoka kosa la jinai la kumtukana askari na kubaki makosa mawili ya barabarani na hivyo kulipa Sh 60 elfu.
Miezi mwili baadaye mfanyakazi mwingine naye alibambikiwa kosa ingawa yeye hakulazwa ndani, lakini alipoteza muda mwingi wa kazi kwenda mahakamani.
Mimi mwenyewe mwezi huu wa Aprili pale makutano ya Morocco nikiambiwa nimepita baada ya taa nyekundu. Nikamweleza kuwa taa nyekundu imenikuta katikati ya barabara kwa vile hakuna taa ya njano ya tahadhari, hivyo sikuweza kusimama katikati.
Kilichoniponza ni kuwa nilikuwa na nafasi kubwa kati yangu na gari ya mbele yangu, ambalo ilikuwa hivyo kwa kuwa nafasi hiyo ilikuwepo toka tunakaribia makutano hayo.
Aidha kuonyesha kuwa sikufanya kwa makusudi kilipita kitambo kati yangu na gari za upande mwingine, lakini askari akaanza kulalamika kwa nini najitetea badala ya kumwomba samahani.
Nilishukuru aliposema aniandikie notification ya kulipa faini maana sikutaka kuingia mtego wa kulipa pesa isiyokuwa na stakabadhi. Lakini mbaya zaidi mtu mwingine alikumbana na tatizo kama la kwangu lakini askari wenzake waliongea naye kidogo na wakamwachia.
Nilipomwuliza huyo askari kwa nini mwenzangu ameachwa akanijibu kuwa huyo hakusimamishwa na yeye. Nililipa faini lakini nikaenda kwa afande ninayemfahamu kumwomba waangalie tatizo la taa za njano makutano ya Morocco maana ni hatari kusimama ghafla katikati ya njia panda hiyo.
Emmanuel Kihaule: Jeshi la Polisi Kitengo cha Trafiki uhakikisha haki inatendeka barabarani bila kutetea dereva au askari husika. Kisa hiki ni ushuhuda mmojawapo. Hongera sana Kamanda Awadhi. Siku zote umekuwa ukifanya kazi kwa weledi wa hali ya juu!
Nakumbuka pia vipo visa kadhaa ambapo Kamanda Mpinga aliwaamrisha askari husika kulipa faini walizowalipisha madereva kimakosa. Cha msingi wote tujitahidi kufuata sheria na pale unapoona umeonewa (lakini hakikisha kweli hujafanya kosa) basi toa taarifa na suala husika litashughulikiwa.
Danny Matiko: Vyema sana! Matukio ya uonevu aina hii ni mengi mno; waandishi tunayafahamu, kamwe tusiyafumbie macho.
John Monia: Balile hongera kwa kuweka wazi tatizo la hawa ndugu. Sisi wengine hatuna sehemu ya kusemea na muda wa kufuatilia.
John Hagu: Afande Awadhii ni mcha Mungu!!
Moustapha Puya: Awadhi na Mpinga wako vizuri. Wana maelekezo mazuri mpaka kama umekosea unaona aibu.
Mdoe Kiligo: Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu. Wote tukipaza sauti Askari wa Usalama Barabarani watarudi kwenye mstari na kufanya kazi kwa misingi ya haki.
Moustapha Puya: Kuna WP mwingine kituo cha Tabata, anabambika makosa, anachotaka yeye ni hela tu, na kitabu cheki feki. Hana mashine wala nini. Yule dada wa Tabata hatari.
Lucas Ishengoma: Kweli Tabata yupo Dada mmoja alinitoza faini kwa kuwa gari yangu ilijaa vumbi ambalo lilitokana na vumbi la Kiwanda cha National Battery pale Pugu Road. Sisi magari yetu huwa yanashinda pale TTCL, kwa hiyo hayo mavumbi hutemwa kutoka kiwandani na kusambaa kwa majirani.
Richard Sawala: Pale external mataa ndio zao kuvizia hata kama taa ya njano imewaka upo katikati unao!!
Majura Mutalemwa: Namfahamu Inspekta Alex Bihemo aliwahi kufanya kazi Kituo cha Polisi Luguruni ni askari anayedhani yeye daraja lake la uraia ni bora kuliko Watanzania wengine!
Na yeye kama msimamizi wa Beatrice alistahili kuchukuliwa hatua kwa kuwa alikuwa anakula njama za kumwonea Leonce Mujumuzi kupitia upotoshaji wa makusudi huku akijua ni kinyume cha sheria!
 Sitanii, michango ya Watanzania hawa kuna ujumbe inaoufikisha. Binafsi naomba kusisitiza. Sikwenda kwa Kamanda Awadhi kuomba atusaidie, bali kuomba haki itendeke. Namshukuru ametenda haki na askari WP Beatrice ameagizwa kulipa fedha hizo.
Nawaomba Watanzania tuendelee kuheshimu sheria za barabarani na tuzitii bila shuruti, ila ukibaini askari amekuonea usipigane, usitukane wala kutoa ishara potofu, ulizia mkuu wake wa kazi eneo aliko na chukua hatua za kiutawala kuwasilisha malalamiko yako. Utasikilizwa, kama una haki itapatikana, kama una kosa utalipishwa faini.
Pia, watu wengi wameniambia askari wanatukana madereva. Si kazi ya askari kumtukana dereva, ukitukanwa na ukawa na ushahidi mchukulie hatua askari husika kwa kufikisha malalamiko yako kwa viongozi wake, haki itatendeka.
Sitanii, sheria zimetungwa kuhakikisha haki inatendeka, si kuonea au kumpendelea mtu. Nathamini na kutambua kazi kubwa wanayofanya askari, ila hao wachache wanaochafua sura ya Jeshi la Polisi waadhibiwe kwa mujibu wa sheria. Asante sana ACP Awadhi.