Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Naibu Waziri ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora Ridhiwan Kikwete amewataka Wakuu wa idara wanaosimamia utawala na rasilimali watu nchini kuacha roho mbaya kwa watumishi wenzao na kufanya kazi zao kwa upendo kwa mujibu wa taratibu kanuni na sheria za utumishi wa umma.
Ridhiwani ameyasema hayo leo mkoani Arusha wakati akifunga mkutano wa 11 wa mwaka wa wanachama wa( AAPAM) tawi la Tanzania na uzinduzi wa jumuiya ya maafisa Tawala na rasilimali watu Tanzania (TAPAHR) .
Amesema wapo baadhi ya maafisa rasilimali katika maeneo yao badala ya kuwasaidia watumishi wenzao wamekuwa vikwazo vikubwa vya kuwasaidia watumishi wanaowaongoza ikiwemo kutoshughulikia malalamiko yao kwa wakati, mfano mzuri ni wilayani Bunda zaidi ya watumishi 700 wamezuiliwa mishahara kwa kutojaza mfumo wa PEPMIS.
“Nina taarifa hapa kuhusu watumishi 700 ambao wamesitishiwa mishahara wilayani Bunda kwa kutojiunga na mfumo wa PEPMIS hilo ni jambo la kushangaza sana hii inaonyesha ni jinsi gani hakuna mahusiano mazuri na watumishi mpaka inafikia hatua hiyo,namuagiza Afisa rasilimali watu wa halmashauri ya wilaya hiyo kufuatilia na kubaini suala hilo na kupeleka maelezo wizarani.”amesema.
“ifike wakati Sasa mbadilike acheni roho mbaya fanyeni Kazi kwa kushirikiana na watumishi wenu ikiwemo kusikiliza changamoto zao na kuzifanyia kazi sio kusubiri hadi waende makao makuu (Wizarani )kwa ajili ya kueleza changamoto zao kule wakati nyie mpo huku na mmepewa dhamana ya kuwaongoza na kusikiliza changamoto zao ‘amesema Ridhiwan.
Aidha ameongeza kuwa, katika Moja ya malalamiko ambayo nimekuwa nikiyapata kwenye ofisi yangu ni watumishi kutopandishwa madaraja wakati wamekaa ofisini muda mrefu na wanastaili kupata haki zao ila kikwazo kikubwa kipo kwa wakuu wa idara wanaosimamia utawala na rasilimali watu.
“Nyie mmekuwa kikwazo kikubwa sana cha kusababisha watumishi wasipandishwe cheo hamtaki kabisa waende kwa Katibu mkuu ili wasipandishwe cheo ,nyie kazi yenu ni kuandika barua na kuituma kwa Katibu mkuu yeye ndio ataamua ampandishe cheo au lah,achane kuwabania wenzenu “amesema.
“Suala la kupandishwa madaraja na kubadilisha muundo ni suala la Katibu Mkuu na sio suala lenu acheni roho mbaya wasaidieni watumishi kuwaandikia barua mambo mengine atafanya Katibu Mkuu mwenyewe msiwabanie watumishi wenu haipendezi” kabisa.”amesema .
Kwa Upande wake Kaimu Katibu Mkuu wizara hiyo Xavier Daudi amesema malengo ya Mkutano huo ni kutoa fursa kwa wataalamu wa usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala na kubaini changamoto katika kusimamia sekta hiyo.
Amesema masuala yote mliojifunza hapa yakifanyika yataketa ufanisi mkubwa sana na kuleta tija sana pia kuweka mikakati ya kusimamia rasilimaliwatu kwa Makubaliano yaliowekwa na AAPAM na nchi wanachama wa Afrika.
Kwa Upande wake Mwenyekiti Mpya wa TAPAHR nchini Grace Meshi ameshukuru kwa kuchaguliwa na ameahidi kutoa ushirikiano sanjari na kupeleka Jumuiya hiyo mbele na kuifanya kuwa ya mfano wa kuigwa na kwamba maelekezo na maagizo ya Naibu Waziri wanaenda kuyafanyia Kazi.