Na Lusungu Helela, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene ameonesha kukerwa na baadhi ya Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi za Serikali wenye tabia ya kuwafokea Watumishi walio chini yao wakiamini kufanya hivyo ndio uongozi.
Amesema baadhi yao hudiriki hata kuwatukana watumishi huku akisisitiza jambo hilo ni kosa kubwa na kama kuna kiongozi anataka kufanya ufanisi lakini anafikia hatua ya kutukana watumishi huyo hafai kabisa kwani zipo kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa umma za kuchukua kama mambo hayaendi sawa
Ametoa kauli hiyo leo wakati alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma katika Kampasi ya Dar es Salaam ambapo amesema hivi vitu ni maslahi ya umma, Kiongozi makini hahitaji kununa wala kufokafoka cha msingi ni kuchukua hatua.
” Kuna watu walikuwa wanasoma bidii zote ili wapate nafasi kwenye utumishi wa umma ili waje wakomeshe watu, kuna watu kazi yao kubwa ni kuwashughulikia watu na hiyo ndo raha yao” ameng’aka Simbachawene
Amesema mshahara hata uwe mkubwa kiasi gani kwa watumishi kama mahali hapo pa kazi hakuna amani, kuna manyanyaso, hakuna kuthaminiwa na kutambuliwa kwa mchango wao hapawezi kuwa na ufanisi wa kazi.
Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Simbachawene amesema akitaka Chuo Cha Utumishi wa Umma kisisubiri kuitwa kitoe mafunzo ya kujengeana uwezo mahali pa kazi pamoja na kuhakikisha kinatoa mafunzo ya awali kwa watumishi wanapoanza kazi ili waweze kutambua haki na wajibu wao.
Amesema huko kwenye Taasisi za Serikali kuna shida kubwa ya migogoro ya watumishi isiyoisha ilhali Chuo cha Utumishi kipo ” nilitegemea kuona mnafika kwenye Taasisi hizo kwa lengo la kutoa mafunzo kwa watumishi ili mambo yaende lakini hamfanyi hivyo”
” Nakutana na mashirika makubwa ya nje yananiomba yakatoe mafunzo ya kuwajengea uwezo katika Taasisi fulani za Serikali wanaona mambo hayaendi sawa ilhali ninyi mpo hii sio sawa changamkeni mna fursa nyingi za kubadilisha utumishi wa umma nchini.
Amesema Chuo hicho kifanye mafunzo ili kuepuka watumishi wengi kupelekana mahakamani au TAKUKURU ilhali Chuo cha Utumishi kupitia mafunzo ya kujengeana yangetolewa ingekuwa ni mwarobaini na hali isingefikia huko.
Awali Mkuu wa Chuo hicho, Dkt.Mabonesho ameishukuru Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mchango mkubwa wa kutatua tatizo la watumishi katika Chuo ambacho kilikuwa kinakabiliwa na uhaba wa watumishi na hivyo kukwamisha kufikia malengo waliyojiwekea.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akizungummza na Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Dar es Salaam.
Baadhi ya Watumishi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene wakati alipofanya ziara ya kutembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akipata maelezo wakati alipotembelea chumba cha mashine za kizamani za kujifunzia za kuchapa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Utumishi Kampusi ya Dar es Salaam akiwa na Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Ernest Mabonesho.
Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Ernest Mabonesho akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene kwa ajili ya kuzungummza na Watumishi wa Chuo hocho Kampasi ya Dar es Salaam
Kwaya ya Chuo cha Utumishi wa Umma ikiimba mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene wakati alipowasili katika Chuo hicho kwa ajili ya kuzungumza na Watumishi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma