“Wivu ni kansa ya akili’’. – B.C. Forbes
Acha wivu. Wivu hautajirishi. Wivu hauna tuzo ya aina yoyote. Wivu ni kubeba msalaba mzito usiokuhusu. Mwandishi B.C. Forbes anasema: “Wivu ni kansa ya akili.” Kama unataka kufanikiwa katika maisha, acha wivu.
Kama unataka kuishi maisha yenye amani, acha wivu. Kama unataka kubarikiwa, acha wivu. Mwenye wivu hana alama usoni. Alama yake imo moyoni. Akiona mwenzake amefanikiwa anaumia sana. Anataka afanikiwe yeye peke yake. Anataka abarikiwe yeye peke yake. Anataka ale keki ya Mungu yeye peke yake. Anataka abaki kileleni yeye peke yake. Anataka apongezwe yeye peke yake.
Hauwezi kufanikiwa kwa kuwaombea wengine wasifanikiwe. Unafanikiwa kwa kuwaombea wengine wafanikiwe. Sala yako iwe: “Mungu naomba fulani afanikiwe,” siyo “Mungu naomba fulani asifanikiwe.”
Yafurahie mafanikio ya mwenzako kwa moyo wa shangwe na vigelegele. Mafanikio ya mwenzako ni mafanikio yako. Yafurahie.
Mwenzako akifanikiwa mpongeze. Ikiwezekana mnunulie zawadi ya kumpongeza. Mtie moyo aendelee kufanya vizuri zaidi. Mwambie: “Songa mbele.” Mwambie: “Mungu ana mpango mzuri na maisha yako. Usikate tamaa.” Mtamkie Baraka. Fufua uwezo wa kuwapenda wenzako.
Macho yako yafundishe kuona mazuri ya wenzako. Bubujikwa machozi ya furaha pale unaposikia habari njema za mwenzako. Tumeumbwa kuyafurahia mema/mazuri ya wenzetu na si kufurahia maanguko yao. Kama una tabia ya kufurahia maanguko ya wenzako, acha. Acha kuchekelea madhaifu ya mwenzako. Ahidi kuacha wivu usio na tija kuanzia leo. Mungu anapokupa nafasi ya kuyajua madhaifu ya mtu mwingine kwa undani, ni kwa sababu amekuamini.
Wainue wengine juu nawe utainuliwa na uliowainua. Mwandishi wa Marekani, Zig Ziglar anasema: “Utapata chochote unachotaka kwa kuwasaidia wengine kupata wanachohitaji.”
Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Kidole kimoja hakivunji chawa. Mwanasayansi Isaac Newton anasema: “Kama nimeona mbali zaidi ni kwa kusimama kwenye mabega ya watu wakubwa.” Ukitaka kwenda kwa kasi tembea peke yako. Ukitaka kufika mbali tembea na watu wengine.
Mwandishi mmoja mwenye hekima aliwahi kuandika: “Ukitaka furaha ya saa moja – lala. Ukitaka furaha ya siku moja – nenda kavue samaki. Ukitaka furaha ya mwezi mmoja – oa au olewa. Ukitaka furaha ya mwaka mmoja – shinda bahati nasibu. Ukitaka furaha ya maisha yako yote – jitoe kwa ajili ya wengine.”
Kujitoa kwa ajili ya wengine ni kuwapenda. Ni kuwasaidia. Ni kuwasikiliza. Ni kuwatetea. Ni kuacha kuwaonea wivu.
Maisha unayoishi yanaitambulisha sura ya nani? Mwanafalsafa Tolmons alipata kuandika hivi: “Katika maisha unaweza kuonyesha sura ya Mungu au sura ya shetani.” Kazini kwako unaweza kuonyesha sura ya shetani au sura Mungu. Kwenye familia yako unaweza kuonyesha sura ya shetani au sura ya Mungu. Kwa majirani zako unaweza kuonyesha sura ya shetani au sura ya Mungu. Inategemea maisha yako unayoishi yanawakilishwa na matendo ya aina gani, kama ni matendo yasiyofaa, basi ni dhahiri kwamba unawakilisha sura ya shetani.
Tupembue tuone. Wivu ni sura ya shetani. Umbeya ni sura ya shetani. Uongo ni sura ya shetani. Uchoyo ni sura ya shetani. Ufisadi ni sura ya shetani. Rushwa ni sura ya shetani. Uchu wa madaraka ni sura ya shetani. Sura ya Mungu ni sura ya uadilifu na uaminifu. Sura ya Mungu ni sura ya upendo. Sura ya Mungu ni sura ya amani. Sura ya Mungu ni sura ya mshikamano. Sura ya Mungu ni sura ya unyenyekevu na huruma.
Ishi na watu vizuri. Ishi na majirani zako vizuri. Kumbuka: Unaishi na watu. Kuzaliwa kwako kumefanywa na watu. Jina lako unalotumia umepewa na watu. Umepata elimu kutoka kwa watu. Kipato chako unachopata kinatoka kwa watu. Heshima uliyonayo inatoka kwa watu. Ulipozaliwa uliogeshwa na watu. Wa mwisho kukuogesha watakuwa watu. Mazishi yako yatasimamiwa na watu. Utapelekwa makaburini na watu. Kila unachomiliki kitarithiwa na watu. Ishi na watu vizuri.
Maisha ni kama sarafu iliyotupwa angani. Huwezi kutabiri itadondokea upande gani. Mtu unayemdhihaki leo na kumwona kama takataka, inawezekana ndiye atakayeamua hatima ya maisha yako kesho. Mwanzoni mwa mwaka 1980 meneja wa hoteli moja ya kitalii huko Hanzghou nchini China alimnyima kazi bilionea Jack Ma (kwa wakati huo Jack Ma alikuwa hana utajiri wa aina yoyote). Baadaye Jack Ma alianzisha Kampuni ya Alibaba na kumwajiri mtu yule aliyemnyima kazi. Maisha ni mzunguko. Ishi katika mzunguko wa kumheshimu kila mtu.