Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo Abdul Nondo amedai kuwa ametishiwa kuuawa endapo atasimulia kilichotokea baada ya kutekwa na wateaji
“Ukitoka hapa nenda moja kwa moja nyumbani kwako. Tunapajua vizuri na usizungumze kokote juu ya kilichotokea, pia tusikuone ukizungumza na vyombo vya habari. Ukifanya hivyo tutakuchukua na raundi hii tutakuua,” amedai Nondo
Amedai kuwa alikamatwa na kuchukuliwa kwa nguvu na watu sita dakika chache baada ya kuwasili katika eneo la Stendi Kuu ya Mabasi jijini Dar es Salaam akitokea Kigoma alipokuwepo kikazi.
Nondo amedai, baada ya kunaswa, waliohusika na tukio hilo walikuwa wakimueleza mara kadha kuwa kuzungumza kwake kumemponza na kwamba huo ndio mwisho wake.
“Wakati wakinipiga waliniambia ‘wewe si cha mdomo’ endelea leo tunakuua,” amedai na kuongeza kuwa waliomteka walimuumiza vibaya kwenye maeneo mbalimbali ya mgongo, mikono na miguu.
Mwanasiasa huyo, amedai kuwa alipowasili katika Jiji la Dar es Salaam, alishtuka baada ya watu sita kumkaba na kumchukua kwa nguvu katika eneo hilo la stendi ya mabasi.
Anasema, “Watekaji walinichukua kwa nguvu, licha ya kelele na vuta nikuvute. sikusaidika na kulikuwa na bodaboda moja na watu wengine wakiangalia tukio lile likiendelea lakini hawakunisaidia.”
Nondo ameongeza kuwa walimuingiza kwenye gari na kuondoka naye. “Walinifunga kitambaa cheusi kwenye macho, kamba mikononi … walinisafirisha kwa mwendo huku nikipigwa na baadaye walininginiza mahali, miguu juu huku wakinipiga kwenye unyao wa miguu, walinipiga mgongo na mikononi,” amedai.
Nondo amedai “Nilitolewa na kubadilishwa kwenye gari nyingine… wakanifungua pingu, wakanifunga kamba na kuniingiza kwenye gari ndogo kutoka ‘hardtop’ kisha kunisukumiza kwenye fukwe hizo…Nilihisi upepo na mawimbi ya bahari.”
Anasema wakaondoka na ndipo alipopata msaada wa kwenda katika ofisi za chama hicho zilizopo Magomeni jijini Dar es salaam.
“Nilikuwa na hali mbaya, sikuweza kwenda nyumbani maana naishi mwenyewe hivyo salama yangu ilikuwa ni kwenda ofisini na ndipo nilipoletwa hospitalini,” anaeleza Nondo.