Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mwenyekiti wa Ngome ya vijana ya chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo amedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana akitokea mkoani Kigoma alikokuwa na viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho, walioongoza kampeni kwenye mikoa ya magharibi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27.

Taarifa za kutekwa kwa Nondo zimetolewa na ACT Wazalendo kupitia taarifa kwa umma iliyosainiwa na Naibu Katibu wa haki za binadamu na vyombo vya uwakilishi wa wananchi, Taarifa hiyo inasema: Nondo aliwasili katika kituo cha basi cha Magufuli eneo la Mbezi kwa usafiri wa basi la Saratonga lenye namba za usajili T221 DKB.

Pia taarifa hiyo imewanukuu mashuhuda wa tukio waliosema kuwa kulikuwa na purukushani katika utekeji wa Nondo uliosababisha mkoba wake wa nguo na pingu iliyobebwa na mmoja wa watekaji kudondoka.

“Katibu Mwenezi wa chama hicho, mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala na Afisa Harakati na Matukio Taifa, Wiston Mogha waliofika mapema kituoni hapo walitambua haraka kuwa aliyetekwa ni Abdul Nondo kwa sababu walizitambua nguo zake kwenye mkoba uliodondoka pamoja na notebook yake”, ilifafanua taarifa hiyo.

Imeongeza: ACT inaendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tukio hilo na taarifa zaidi itatolewa. Chama hicho kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus Wambura, kufuatilia haraka tukio hilo na kuhakikisha Bw. Nondo anaachiwa huru mara moja.

Hata hvyo taarifa ya Jeshi la Polisi limesema kuwa, majira ya saa 11 alfajiri katika stendi ya Magufuli jijini Dar es Salaam, kuna mtu mmoja mwanaume amekamatwa kwa nguvu na kuchukuliwa na watu waliokuwa wakitumia gari lenye usajili T 249 CMV aina ya Landcruiser rangi nyeupe.

Polisi imesema mashuhuda walieleza kuwa vitu vilivyodondoshwa na baadhi ya vitu vilivyokuwemo kwenye mkoba vimetambuliwa ni vya Abdul Omary Nondo.

Polisi imesema kuwa ufuatiliaji wa tukio hilo ulianza mara tu baada ya kupokelewa kwa taarifa ya Polisi, sambamba na kufungua jalada.