Nina uhakika wale mashabiki wa Bendi ya DDC Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ Ngoma ya Ukae’ wakati huo – vijana wa zamani, watakuwa wanakumbuka mbali kila pale linapotajwa jina la mwanamuziki Abdallah Gama.

Gama ni mkung’utaji mahiri wa gitaa la kati (rhythm), aliyepata kusumbua akili za wapigaji magitaa wengine wengi enzi zile, hususani alipokuwa katika bendi hiyo ya Sikinde.

Nguli huyo ni miongoni mwa wanamuziki 12 ambao mwaka 1978 walijiengua kwenye kundi la Dar International kwa madai ya kupinga uongozi mbovu wa mmiliki wao, Zachariah Ndabameiye, na kuanzisha Bendi ya Mlimani Park Orchestra.

Imeelezwa kuwa baada ya kujiengua walikwenda kuungana na wanamuziki wengine akina Abel Bartazar, George Kessy, Haruna Lwali na Ibrahim Mwinchande na kuwa waanzilishi wa Bendi ya Mlimani Park Orchestra.

Baadhi ya wanamuziki wengine waliochomoka Dar International na kwenda kuanzisha bendi hiyo walikuwa ni King Michael Enock (Teacher), aliyekuwa mtaalamu wa kupiga ala zote za muziki, Cosmas Chidumule, Joseph Mulenga ‘King Spoiler’, Machaku Salum, Joseph Bernard na Habib Jeff.

Wakati akiwa kwenye Bendi ya Dar International aliyoitumikia kuanzia mwaka 1977, Gama alishiriki kupiga rhythm kwenye vibao vingi, baadhi yake vikiwa ni ‘Sikitiko’, ‘Mwana Rudi Uoe’ na ‘Mwalimu Nyerere’.

Alipoingia katika bendi hiyo ya Mlimani Park Orchestra, Gama, kwa kipindi kifupi alijipatia umaarufu mkubwa, hasa kwa umahiri aliokuwa nao katika kulicharaza ipasavyo gitaa la hilo kwenye vibao vingi vya bendi hiyo.

Gama ni mwanamuziki aliyefaulu kwa kiasi kikubwa kuzigusa nyoyo za mashabiki wengi kutokana na tungo zake zenye maudhui maridhawa  yaliyoshiba ujumbe mzito, za ‘Hadija’, ‘Dar es Salaam Airport’, ‘Maudhi ya Nyumbani’, ‘Linda’ na ‘Nawashukuru Wazazi’.

Akielezea wasifu wake Gama alianika mambo mengi hususani historia yake kimuziki na maisha kwa ujumla.

“Baba yangu aliyekuwa fundi cherehani, ndiye aliyenivuta kwenye muziki kwani alikuwa akipiga gitaa lisilotumia umeme la galatoni, kujifurahisha na wakati mwingine akiwaburudisha rafiki zake,” anasema Gama.

Alisema kuwa akiwa na umri wa miaka 28, alikuwa tayari anafahamu kikamilifu jinsi ya kulikung’uta gitaa. Bendi yake ya kwanza kupigia ilikuwa ni Safari Trippers aliyojiunga nayo mwaka 1973.

“Nikiwa Safari Trippers nilishiriki kupiga gitaa la solo kwenye vibao kadhaa, vikiwamo ‘Ooh Lila’ na ‘Mateso’ ambavyo vyote ni matunda ya Marijani Rajabu,” alibainisha Gama.

Ni mwanamuziki asiyependezwa na tabia ya wanamuziki kuhamahama na makundi. Mwaka 1975 alijiunga na bendi ya Tanzania Stars ambayo maskani yake yalikuwa katika Hoteli ya Margot iliyokuwa katika mtaa wa Independence (siku hizi ni Samora) katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Lakini hata hivyo, mwaka 1984 Gama alijiunga katika Bendi ya Bima Lee iliyokuwa ikimilikiwa na Shirika la Bima la Taifa (NIC).

“Nikiwa na Bima Lee iliyokuwa ikipiga muziki kwa mtindo wa ‘Magnet tingisha’ nilitunga kibao cha ‘Fungua Macho’ pamoja na kushiriki kucharaza gitaa kwenye vibao kama vile ‘Makulata’ na ‘Tujemaso,” anafafanua Gama.

 

>>ITAENDELEA

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0767 331200, 0784  331200 na 0713 331200.