Na Cresensia Kapinga, Namtumbo.

Abate wa Abasia ya hanga jimbo kuu katoriki la Songea mkoani Ruvuma amechangia kiasi cha Sh. Milioni 25 kwaajili ya ujenzi wa nyumba ya mwalimu wa Madrsa katika kijiji cha Mtakanini kilichopo Wilayani Namtumbo mkoani humo.

Abate Octavian Masingo ametoa mchango huo kwenye harambee ya ujenzi wa nyumba ya mwalimu wa madrasa iliyoendeshwa na Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete iliyofanyika wakati wa ufunguzi wa msikiti wa Masjid Taqwa uliojengwa katika kijiji cha Mtakanini na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi wakiwemo viongozi mbalimbali wa dini, chama na serikali.

Katika harambee hiyo pia walijitokeza kuchangia nyumba ya mwalimu wa madrasa, Makamu mwenyekiti wa chama cha mapinduzi Bara Abdrahaman Kinana na mkurugenzi mstaafu wa usalama wa Taifa Rashidi Othumani pamoja na kaimu Kadhi Mkuu sheikh Ali Mkoyogole ambaye pia alikuwa mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa msikiti huo wa Masjid Taqwa ambao jengo lake ni la kisasa ambapo katika harambee hiyo zaidi ya Sh. Milioni 168 zimepatikana.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo ya ufunguzi wa msikiti ambayo ilihudhuriwa na mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas, Rais Mstaafu Dkt. Kikwete amesema kuwa kitendo kilichofanywa na Ramia Yasin cha kuamua kujenga msikiti ni kitendo cha kuigwa na watu wengine ambao wengi wao wanakuwa na uwezo mkubwa lakini hawakumbuki kujenga nyumba za ibada kwani nyumba za ibada ni kiungo kikubwa cha kutoa taaluma mbalimbali kwa watu na kiunganishi kati ya watu na Mungu.

Msitaafu Kikwete amewahimiza wananchi kuona umuhimu wa kumtolea Mungu sadaka pale wanapokuwa na mafanikio na kwamba sadaka nzuri kwa Mwenyezi Mungu ni kumjengea nyumba ya Ibada kama alivyofanya Ramia Yasini na si vinginevyo.

Ametoa wito kwa wananchi kuona haki ya kusaidia jamii iwe ya kiimani ama ya kimaendeleo lakini pia itawajengea watoto kimalezi kukuwa kiimani zaidi na kuendelea kumpenda Mungu.

Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa chama cha mapinduzi Taifa bara (CCM) Abdrahmani Kinana amesema kuwa binadamu yeyote mwenye tabia njema anakua mcha Mungu mnyenyekevu,mpole,mwenye huruma na mkarimu kwa jamii inayomzunguka hivyo ni vyema kuendelea kumtolea Mungu sadaka.

Naye mkurugenzi mkuu mstaafu wa usalama wa Taifa Rashid Othuman amewahimiza wakazi wa kijiji cha mtakanini kutunza nyumba hiyo ya ibada badala ya kuacha msikiti ukichakaa mpaka kufikia hauta ya kuota nyasi jambo ambalo sio jema na badala yake wananchi wa kijiji hicho pamoja na vijiji vya jirani wanapaswa kuutumia vizuri kwa kwenda kumuabudu Mungu ili kuongeza zaidi imani zao.

Hata hivyo Ramia Yasin ambaye ndiye aliyejenga msikiti huo wa kisasa amewashukuru wazazi wake pamoja na walezi wake , marafiki zake ambao wekiwemo wafanya biashara kwa kumpa moyo wakati anajenga msikiti huo wa masjid Taqwa kwa ushauri amabo ulimfanya asikate tamaa mpaka kufanikiwa kuumaliza na anaendelea kumshukuru Mungu kwa mafanikio yaliyo mbele yake.