Baada ya kuonesha mifano miwili hiyo kuhusu uwajibikaji ulivyokuwa katika nchi yetu enzi za Mwalimu, sasa turudi kwenye hali ya sasa ya kuporomoka kwa maghorofa hapa jijini Dar es Salaam.

 

Niliwahi kusoma katika Gazeti la JAMHURI la Aprili 02-08, 2013 Uk. 3 nukuu za baadhi ya maneno ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Pinda bungeni Dodoma mwaka 2008.

 

Baadhi ya matamko yake yalikuwa kama “can you imagine mtu anaamua kupandisha ghorofa lake hapo bila kufuata taratibu za mamlaka husika, ni hatari kubwa!” Tena kuna matamko kama, “…ni lazima Serikali tuingilie kati Dar es Salaam, lile jiji ambalo ni kioo cha Taifa letu…”

 

Hatua zipi zimechukuliwa kuzuia uvunjaji wa sheria za ujenzi? Kama Serikali ingechukua hatua wakati ule ule (acted promptly then) wala yale maghorofa matatu yaliyoporomoka mwaka 2008 na huu 2013 kusingetokea maafa mengine nchini. Kwa kutokuwajibika mtu yeyote leo hii tumepoteza wenzetu 36 jijini Dar es Salaam.

 

Kwa mtazamo wangu, nafikiri sisi wananchi sote tuna kasoro kubwa katika kusaidia Serikali kusimamia sheria za nchi. Inatokeaje kila kata ina Serikali ya Mtaa! Kila nyumba 10 kwa utaratibu wetu kuna mjumbe wa nyumba zile, ndiyo kusema kuna uongozi unaoeleweka. Hapo ndipo ninapojiuliza; inatokeaje sheria za utawala bora zinavunjwa?

 

Watu wanaporomosha majumba tunayaona lakini hakuna kiongozi anayethubutu kuuliza vibali vya ujenzi ule? Majumba yanafumuka kama uyoga, lakini wala hayupo wa kuhoji. Kila mtu anajifanya hahusiki kabisa (no concern whatsoever).

 

Tuchukue mfano rahisi wa matukio ya kila siku katika mitaa yetu. Suala la takataka! Kila mtu anatupa takataka zake ama katika mtaro wa karibu, au kando ya barabara.

 

Hapo hakuna anayeshituka kwa hilo. Sasa mvua ikinyesha tu, ile mitaro inajaa maji na yanatuama. Wadudu wanazaliana katika maji yale na harufu mbaya inatokea. Basi hapo kila mtu anakuwa mwepesi kulalamikia Serikali katika runinga kipindi kile cha ‘Jiji Letu’ katika ITV, unaona na kusikia kila mtu anailaumu Serikali.

 

Utasikia ‘Serikali yetu ituzibulie mitaro yetu’, ‘Serikali ituondolee takataka hizi tunakerwa na harufu mbaya’. Lakini watupaji wa hizo taka ni hao hao wananchi, walalamikaji katika runinga ni hao hao, hapa ndipo mimi nasema kila mtu anao wajibu fulani katika nchi hii.

 

Kuilaumu Serikali kwa kila uzembe wa mtu si sawa sawa. Elimu ya uraia inakosekana, maadili mema hayapo, utawala bora hakuna. Kila mwananchi anapaswa kuwajibika katika nafasi yake na mahali pake. Serikali ni mimi na wewe.

 

Inasifika miji kama Moshi au Jiji la Mwanza ni safi kabisa. Nani kaajiriwa kusimamia usafi huo? Hakuna. Kilichotokea huko ni kila mtu kuwajibika kutunza mazingira ya mji safi. Mamlaka husika zinatoa sera, wanatunga sheria na kuweka kanuni za utekelezaji. Kuanzia hapo kila mtu, kila mkazi na kila mwananchi anawajibika kufuata miongozo inayotolewa kuleta ufanisi katika utawala bora.

 

Katika kufukua kifusi pale mtaa wa Indira Gandhi, Wachina walioshiriki walisema zege la pale halikuwa na saruji ya kutosha ni mchanga mtupu. Hii inaonesha upo uchakachuaji wa hali ya juu katika majengo haya yanayoporomoka.

 

Mamlaka husika kama mipango miji hakuna integrity, wahandisi hawana integrity na wakaguzi majengo hawana integrity ndiyo sababu hakuna mamlaka yoyoye inayoonekana kuhusika na ujenzi huo holela. Nani basi katika hali ya namna hii anaweza kuwajibishwa? Ni Manispaa yote? Hili haliwezekani! Unampembuaje mhusika  “how do you single out” kutoka katika mamlaka hizo?

 

Labda niseme tu kuwa zipo kila dalili tena bila hata chembe ya shaka, ujenzi wa namna hii unatokana na kitu RUSHWA ya hali ya juu. Ewe msomaji wangu, ulimwenguni kuna mambo hujirudiarudia tangu dunia ilipoumbwa hadi kitakapofika kiama.

 

Kwa Wakristo, labda tu tukumbushane katika kitabu kile cha Mhubiri (au Kohelethi) kuna maneno: “….yaliyokuwako ndiyo yatakuwako na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua” (Mhu. 1:9).

 

Maneno haya yanakumbusha kuwa katika ulimwengu huu chini ya jua hili, hakuna jambo lolote jipya linalotokea ambapo hapo kale halikupata kutokea.

 

Kwa mtazamo wa namna hii, mimi nasema mambo kama haya ya rushwa ulimwenguni hata enzi za Wayahudi yalikuwapo na Mungu aliyakemea vikali. Mungu alitumia maneno haya kwa viongozi wa nyakati zile: “Usipotoe maamuzi; wala usipendelee uso wa mtu, wala usitwae RUSHWA; kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya wenye akili na kugeuza dawa ya wenye haki? Yaliyo haki kabisa ndiyo utakayoyafuata ili upate kuishi na kuirithi nchi upewayo na Bwana, Mungu wako” (Kumb. Sura 16 mistari 19 – 20).

 

Kama majengo haya yangelijengwa kwa mujibu wa sheria na kwa haki, hakungelitokea ripoti ya kusema ujenzi haukufuata sheria na kanuni za ujenzi. Pia kama vibali vilitolewa kihalali ripoti isingelisema majengo 22 hawakupatikana wamiliki wake!

 

Mamlaka zote husika na viongozi wale waliokuwa na dhamana ya kusimamia na kukagua ujenzi ule wangejitokeza kutetea uamuzi wao na wangeliwajibika ipasavyo. Serikali iwaadabishe, itaifishe majengo yasiyo na wenyewe na izuie kabisa hali ya watu kujifanyia wanavyotaka.

 

Hivi karibuni hapa nchini kumetokea sokomoko kweli kuhusu matokeo ya mtihani wa kidato cha IV mwaka 2012. Kelele za jazba zimesikika kudai Waziri wa Elimu awajibike, ajiuzulu. Lakini je, tumetoa uamuzi sahihi hapo au ni mikandamizo ya kisiasa tu?

 

Tukitafakari maoni yaliyotolewa katika gazeti la JAMHURI toleo na. 73 la Jumanne Aprili 2 – 8, mwaka huu Uk. 13, nadhani tutakuwa na busara kidogo na kutafakari upya uamuzi wetu. Kuna maoni ya Dk. Kitila Mkumbo, pale yanauliza “ni sekta gani katika nchi hii matokeo yake yangebandikwa ingefaulu? Kisha kuna “comment” pale inasema, “tupo hoi kuliko tunavyojifikiria katika sekta zote. Hata ungefanya leadership audit ya viongozi wetu katika nyanja mbalimbali sijui wange-score wangapi?”

 

Maoni haya yanathibitisha kuwa uozo wa kutokuwajibika uko katika kila sekta. Kwa maana hiyo uwajibikaji hakuna. Na ndiyo tukubali kuwa Watanzania kwa ujumla wetu tumepoteza “integrity” kabisa.

 

Kutokana na hali hiyo, basi hatuwezi kuaminika, hatukubaliki na tumejijengea mazingira mabaya kweli. Taifa lisiloaminika ni taifa jepesi katika ulimwengu.

Nini kimetufikisha hapo? Ni ile tabia ya kuleana, kuoneana haya na kubebana maadam “tulianza naye basi na aendelee?” Hili limeathiri sana uwajibikaji katika nchi hii. Kila mwenye dhamana awajibike ipasikanavyo.

 

Hatimaye Mei 3, 2013 Serikali kupitia kauli iliyotolewa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Mheshimiwa William Lukuvi, aliwaeleza wabunge na wananchi kwa ujumla kuwa “SERIKALI IMEFUTA MATOKEO YA KIDATO CHA IV YA MWAKA JANA (2012)” na kuliagiza Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kuandaa matokeo mapya kwa kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011.

 

Hii maana yake Serikali imewajibika! Huko kuwajibika kwa Serikali kunadhihirisha ukomavu wa demokrasia katika taifa hili. Basi ni alama ya ile integrity ya Taifa. Utawala wowote ule unaofuata sheria unawajibika ili kuleta haki kwa wananchi wake.

 

Ninaamini hali ya mitihani katika nchi hii haitavuja tena na matokeo hayatavurundwa tena. Baraza la Mitihani litaona umuhimu wa kuwa makini na kuwajibika kwa Taifa hili. Na sote tufuate sheria za nchi katika kila jambo. Tuwe na utamaduni wa kufuata sheria “the rule of law” katika Taifa letu.

 

“MUNGU IBARIKI TANZANIA, HEKIMA UMOJA NA AMANI, HIZI NI NGAO ZETU”.