Wiki hii Serikali inatarajiwa kuwasilisha bajeti bungeni mjini Dodoma. Bejeti hii inakisiwa kuwa ya wastani wa shilingi trilioni 15. Hili ni ongezeko la wastani wa trilioni 2 kutoka trilioni 13 za mwaka jana. Kiasi hiki ni kikubwa mno kwa takwimu. Kinawafanya Watanzania kuwa na matumaini makubwa ila yapo yanayotusikitisha.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, bajeti ikiishafikia hatua hiyo, wabunge hawana namna isipokuwa kuipitisha. Mambo mawili yanaweza kutokea. Kuipitisha bajeti au kuikataa kama ilivyo. Kuipitisha ni salama kwa wabunge na kutoipitisha ni hatari kwa wabunge kwa mujibu wa sheria. Wakiikataa maana yake ni kwamba Rais anavunja Bunge.
Tumeanza na ufafanuzi huu kwa nia ya kueleza na kuwasihi wabunge wawe makini katika kujadili na kupitisha bajeti inayowasilishwa Alhamisi wiki hii. Tunapenda kueleza masikitiko yetu kwa bajeti hii. Kwamba wakati bajeti inawasilishwa ni wazi kuwa hadi sasa hakuna mfumo wa kupitia bajeti iliyopita kufahamu imetekelezwa kwa kiwango kipi.
Kuna mikoa tuna ushahidi kuwa ilitengewa fedha za Kilimo Kwanza wastani wa Sh bilioni 10, lakini kilichotokea hadi mwaka huu wa fedha unaisha, wamepokea Sh bilioni 3 na ushei hivi. Zipo wizara ambazo hivi tunavyokaribia kusomewa bajeti ya mwaka wa 2012/2013, kwa wastani zimepokea chini ya asilimia 50 ya fedha zilizotengewa katika bajeti iliyopita.
Hali hii inatutia shaka. Miradi mingi ya maendeleo imekwama. Bajeti inayotengwa inageuka kiinimacho. Zinatajwa takwimu kubwa kubwa kuvutia wapigakura, lakini uhalisia bajeti tunayotumia kama taifa inaelezwa kuwa si zaidi ya Sh trilioni tano. Tatizo ni kwamba kiasi cha makusanyo kinachokisiwa hakifikiwi, na wakati mwingine wafadhili nao wamekuwa chimbuko la ahadi hewa.
Sisi wa JAMHURI tunasema umefika wakati sasa kama taifa tujadiliane. Tuulizane tuna sababu zipi za kutenga bajeti kubwa tuliyo na uhakika kuwa haitatekelezeka. Bajeti hii iliyotengwa ni ya starehe ya aina yake. Matumizi ya wakubwa ni asilimia 70 na miradi ya maendeleo ni asilimia 30 tena inategemea wafadhili.
Tunafahamu wabunge wengi hawana ujasiri wa kuikataa bajeti hii na kuzua mtafaruku wa kuvunja Bunge, ila kinachoweza kufanyika ni kuhoji mwaka jana bajeti iliyopitishwa ni fedha kiasi gani ziliwafikia walengwa? Utashangaa kuona miundombinu na Tanesco waliotengewa bajeti ya ziada, lakini hadi leo fedha hizo hawajazipata!
Kwa sasa nchi inaendeshwa kwa utaratibu wa funika kombe mwanaharamu apite. Hatudhani kama mfumo huu ni sahihi na salama kwa ustawi wa jamii. Tunawataka wabunge kuhakikisha kuwa zamu hii kabla hawajapitisha bajeti ya mwaka huu, wahoji bajeti iliyopita zilikusanywa fedha kiasi gani na walengwa walipokea nini. Baada ya hilo, tulenge kuishi bila kutegemea wafadhili. Hivi tukitenga bajeti bila kukinga mkono kwa wafadhili nini kitapungua? Tubadilike.