Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amewataka watanzania wasiogope kuwa wajasiriamali wa kilimo kwani kinalipa.

Amesema hata kilimo cha uyoga kimewanufaisha wajasiriamali wengi akiwemo Esther Shebe ambaye amenufaika na mafunzo ya kuendeleza ujuzi kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Ameyasema hayo leo wakati alipotembelea TEA kwenye hafla ya kufunga maonyesho ya kitaifa ya kazi za utamaduni na Sanaa yaliyokuwa yakifanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Akiwa kwenye banda hilo baada ya kusikiliza mafanikio ya mjasiriamali huyo, Waziri Kabudi aliwataka watanzania wasiogope kufanya ujasiriamali wa Kilimo kwani wanaweza kunufaika kama Shebe ambaye amemudu kutengeneza bidhaa mbalimbali zinazotokana na Uyoga.

“Nimefurahi sana kuona namna ulivyoweza kutengeneza bidhaa nyingi kwa kutumia uyoga nahamasiha na wengine wafanye kama wewe wajiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa namimi naahidi nitakuwa mteja wako,” alisema kabudi

Shebe anayemiliki kampuni ya Goba Mushroom Zone, alimweleza Waziri kuwa kupitia kilimo cha uyoga amepata mafanikio makubwa ikiwemo kupata tuzo ya kuwa malkia wa nguvu na mkulimo bora wa mwaka 2021.

Picha mbalimbali wakati Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi alipotembelea banda la Mamlaka ya Elimu TEA alipokwenda kufunga maonyesho ya kitaifa ya Sanaaa leo

Alisema yeye alikuwa mkulima kwa miaka mingi lakini mwaka 2022 alikwenda kuongeza ujuzi kupitia Mamlaka ya Kuwendeleza Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) kupitia mfuko wa SDF ambayo yamemwezesha kutengeneza bidhaa mbalimbali.

“Natengeneza bidhaa mbalimbali kutokana na uyoga, nina maabara yangu ambayo naitumia kutengeneza mbegu za uyoga ambazo nauza na zingine nazipanda kwenye shamba langu mwenyewe,” alisema

Alisema mwaka 2023 alipata cheti cha mkulima bora Mkoa wa Dar es Salaam Kanda ya Mashariki na mwaka 2024 alipata tuzo ya kampuni bora ya kilimo na aliishukuru TEA kwa namna ilivyomwezesha kupata mafunzo ambayo yamempa mafanikio makubwa.

“Niliwahi kwenda China kwa mafunzo ya muda mfupi kuongeza ujuzi kupitia chuo cha Sokoine cha Morogoro. Watu wasiogope kilimo kinalipa kwasababu mimi nilikuwa nimeajiriwa Napata mshahara ambao ulikuwa hautoshi lakini kipato changu kwa sasa kinatosheleza mahitaji yangu,” alisema