Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Kufuatia jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya elimu na kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwepo, walimu wanapaswa kuwa wabunifu na kuimarisha utoaji elimu bora ili kuinua taaluma kwa wanafunzi.
Rai hiyo imetolewa April 29,2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Wilson Mahera, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI wakati akifunga mafunzo ya matumizi bora na salama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule na Walimu, yaliyofanyika Kibaha, Mkoani Pwani kwa udhamini wa Mradi wa Boost .

Alieleza, usimamizi makini wa walimu ni kichocheo muhimu cha uboreshaji wa elimu nchini.
“Walimu wana deni la kuwapatia wanafunzi elimu yenye ubora unaostahili, kwani serikali tayari imefanya kazi kubwa ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia,” alieleza Mahera.
Mahera alisisitiza pia wajibu wa walimu katika kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa aina mbalimbali, hasa wa kijinsia, akieleza kuwa suala hilo ni sehemu ya kuhakikisha taifa linalea kizazi salama chenye maadili.
Aidha Mahera aliwataka viongozi wanaosimamia sekta ya elimu kuanzia ngazi ya Mkoa hadi shule kuimarisha usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji.

Alifafanua mafunzo hayo yanapaswa kuwa chachu ya mabadiliko chanya na ameonya dhidi ya matumizi mabaya ya vifaa vya TEHAMA, akieleza vifaa hivyo vinapaswa kutunzwa .
Vilevile alizitaka Halmashauri zote kutenga bajeti maalum kupitia mapato ya ndani ili kuanzisha vituo vya walimu vitakavyowezesha mafunzo endelevu ya kila mwezi.
Alitoa wito kwa kila mkoa na halmashauri kuhakikisha shule zote za kutwa zinatoa huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi ili kuboresha usikivu darasani.

Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Awali kutoka TAMISEMI, Suzanne Nusu, alisema ,washiriki 1,800 wakiwemo Maafisa Elimu Kata 600, Wakuu wa Shule 600 na Walimu wa TEHAMA 600 kutoka Halmashauri 184 walishiriki kwenye mafunzo hayo kwa lengo la kuinua kiwango cha matumizi ya TEHAMA katika shule za msingi na sekondari.
Ofisa Elimu wa Kata ya Murusagamba, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Catherin Herintee, aliishukuru Serikali kwa mafunzo hayo kupitia Mradi wa Boost .

