Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Sallaam

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amewatoa hofu wanamichezo nchini mara baada ya uwanja wa Benjamin Mkapa kufungwa hivi karibuni kupisha ukarabati kuchukua nafasi.

Uwanja wa Benjamin Mkapa umekuwa ukitumika kama uwanja wa nyumbani kwa vilabu vikubwa nchini vya Simba na Yanga katika mashindano ya kimataifa.

Serikali kupitia Wizara yake inayohusika na michezo ilitangaza kuufungia uwanja huo wiki mbili zilizopita huku sababu ikitajwa kuwa eneo la kuchezea lilipata athari mara baada ya mchezo wa robo fainali mkondo wa pili kati ya Simba na Al-masry kutoka nchini Misri.

Naibu waziri, Hamisi Mwinjuma amefanya ziara ya ukaguzi katika uwanja huo kujionea mwenendo wa ukarabati unavyoendelea uwanjani hapo.

Kupitia ziara hiyo,Mwinjuma alikutana na wasimamizi wa ujenzi uwanjani hapo na kufanya nao kikao kubaini kasi ya ukarabati inavyokwenda uwanjani hapo.

Akizungumza Mwinjuma mara baada ya ukaguzi kukamilika amewatoa hofu watanzania kuwa wasiwe na shaka yoyote kuhusu fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika kuchezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Tumeona kasi ya ukarabati na ni mambo kadhaa ambayo yanaendelea na ukarabati ila matengenezo haya tunaamini kuwa yatakamilika kabla hata ya tarehe ya mchezo wa fainali kufika.” alisema.

Baadhi ya matengenezo yanayoendelea katika uwanja wa Benjamin Mkapa yamekuwa yakihusisha maeneo mbalimbali yakiwemo majukwaa, eneo la kuchezea, ufungwaji wa vifaa vipya kwaajili ya waamuzi pamoja na ukarabati katika vyumba vya kubadilishia nguo.

Aidha Mwinjuma ameongeza kuwa Serikali inafanya na itaendelea kufanya kila linalohitajika kufanywa kuhakikisha mchezo wa fainali unachezwa katika uwanja huo na hatimae kombe hilo la Afrika linabaki nyumbani.

Klabu ya Simba itacheza fainali ya kombe hilo la Shirikisho Barani Afrika na klabu ya RS Berkane kutoka nchini Morroco.

Mechi ya mkondo wa kwanza wa fainali hiyo inatarajiwa kuchezwa nchini Morroco tarehe 17 mwezi Mei na kisha mechi ya mkondo wa pili wa fainali hiyo ikitarajiwa kufanyika Mei 25 jijini Dar es salaam.