Na Lookman Miraji
Mashindano ya vilabu ya taifa kwa mchezo wa kuogelea yamefikia hatamu hapo jana, Aprili 27 jijini Dar es salaam.
Mashindano hayo ambayo ni sehemu ya kalenda ya chama cha kuogelea nchini yamejumuisha vilabu vya mchezo huo kutoka mikoa minne hapa nchini.
Idadi ya zaidi ya waogeleaji 100 kutoka vilabu tofauti wameshindana na baadhi ya waogeleaji hao kufanikiwa kuvunja rekodi za zamani na kuweka rekodi mpya ambazo hazikuwahi kuwekwa hapo kabla.
Mashindano hayo yalikuwa ni ya siku mbili Aprili 26-27 yalifanyika katika bwawa la kuogelea la shule ya sekondari ya IST masaki jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yalihitimika kwa timu maarufu za mchezo huo kufanya vizuri na kutunukiwa medali za ushindi.
Matokeo ya jumla katika mashindano hayo yalihitimika kwa klabu ya Taliss IST kuibuka mabingwa kwa kujikusanyia pointi 456, huku nafasi ya pili ikienda kwa klabu ya Dar swimming ambayo iliondoka na jumla ya point 354 huku nafasi ya tatu ikienda kwa klabu ya Reptide kutoka jijini Arusha iliyojikusanyia pointi 55.
Mbali na matokeo hayo ya jumla pia waogeleaji Crissa Dilip, Aryiel Angemi pamoja na Nicolene Violene walifanikiwa kuandika historia ya kuweka rekodi ngumu katika vipengele tofauti ambazo hakiwahi kuwekwa hapo kabla.


