Na Joseph Mihangwa, JamhuriMedia, Shinyanga
“Waasi wa Serikali, wengi kuliko wa dini, wengi hawaendi kusali, lakini wana imani, ambayo kwamba kamili, bila kasoro moyoni. Kama haba ya adili, Serikali huwa chini, ikawa yatenda feli, za shari na nuksani, na dhuluma na batili, na uhaba wa hisani; Kama hawaoni kweli, ni wepesi wa kuhuni; kitu duni Serikali, iwapo mbele ya dini.”
Ni maneno yaliyomo katika shairi; ‘UASI’, la gwiji wa fasihi nchini, Shaaban Robert. Mithili ya gwiji la fasihi la Uingereza, William Shakespeare, Shaaban Robert anabainisha kuwa duniani kote waasi wa Serikali ni wengi kushinda wanaoasi katika dini zao.
Anasema, chanzo cha uasi ni uhaba wa maadili miongoni mwa watawala na hivyo kujipunguzia heshima kwa kuongoza kwa dhuluma, ubatili na ukosefu wa wema.
Matokeo yake ni watu kuhuni au kusaliti Serikali, na kwamba mbele ya dini, Serikali ni kitu kidogo sana. Ukuu wa dini, yaani imani ya mtu, dhidi ya Serikali, inathibitishwa na ukweli kwamba watawala wote hupaswa kuapa kwa misahafu kabla ya kushika madaraka.

Nimelazimika kuanza makala na shairi la Shaaban Robert kutoka kitabu cha: ‘Diwani ya Shaaban: Kielelezo cha Fasili’, ili kujenga hoja kwamba, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika maisha yake ya kisiasa na kidini, alikuwa muasi pande zote.
Kisiasa leo angeitwa ‘mhaini’ na adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa. Kidini angeitwa ‘mjadhambi’ kwa kukashifu au kukufuru dini na Mungu, ambapo adhabu yake ingekuwa ni kutengwa na Kanisa. Lakini yote mawili hayakumtokea.
Kisiasa alikuwa mweledi mkubwa wa kutetemekewa kimataifa; kidini alikuwa mcha Mungu mwenye imani kubwa isiyohojika kwa wema hivi kwamba leo, Kanisa Katoliki linaendesha mchakato wa kumtangaza kuwa Mtakatifu.
Kisiasa, japo alichagua harakati za kudai uhuru wa Tanganyika kwa njia ya amani bila kumwaga damu, lakini kitendo cha kuwatukana Wakoloni wa Kiingereza kwa lugha kali, ya dharau na kuwadhalilisha mbele ya wananchi, ilitosha kumuingiza matatani kwa kosa la ‘uhaini’.
Neema ya wasi, uhaini kisiasa
Wakati mmoja Mwalimu alichochea mgomo wa nchi nzima kwa Watanganyika kususia kunywa bia, akiwaambia kuwa kufanya hivyo ilikuwa ni sawa na kunywa damu ya ndugu zao waliotumikishwa viwandani chini ya mfumo wa uchumi wa kikoloni. Mgomo ukafinikiwa.
Ingekuwa leo, angeitwa ‘mhujumu uchumi’ kama si ‘gaidi’ mwenye nia ovu ya kuharibu amani, utulivu na mazingira mazuri kwa wawekezaji wa kigeni tunaowatetemekea.
Akihutubia Chuo Kikuu cha Toronto, Canada, Oktoba 2, 1969, Mwalimu alisistiza umuhimu wa Mapinduzi kama moja ya nyenzo za maendeleo kwa kusema kwamba, ingawa amani katika mambo ya siasa na ya maisha ya watu ni muhimu, (lakini) ukitaka uwepo uhuru kwa mtu binafsi au kwa taifa katika hali yetu (ya sasa) Mapinduzi ni jambo muhimu katika kudumisha uhuru.
“Kwa kifupi mabadiliko huchafua amani; lakini Mapinduzi ya maana hayawezekani bila kuwako amani. Na amani yenyewe haiwezi kupatikana bila Mapinduzi.
“Mapinduzi maana yake ni vita; na kwamba vita huzaa shida nyingi na mara nyingi wanyonge ndio wanaoteseka zaidi. Tunaamini kwamba kama mlango (wa maendeleo kwa wote) umefungwa, juhudi zifanywe kuufungua; kama umefunguka kidogo, basi lazima usukumwe zaidi (kwa matumizj ya nguvu) mpaka uwe wazi kabisa.
“Kama nafasi hiyo ipo basi si vizuri kuulipua na kuua baadhi ya waliomo ndani kwa kufanya hivyo. Lakini kama mlango wa uhuru (na haki za raia) umefungwa kabisa na kutiwa komeo, na wale wanaolinda wanakataa kabisa kufungua kufuli au kuchomoa komeo, njia iliyobaki haina ma bishano tena, ama mtu unakubali kuukosa uhuru, au unavunja mlango,” anasema Mwalimu.

Anachosema ni kwa umma kutumia nguvu ya wingi wao dhidi ya tawala dhalimu zisizojali uhuru na haki za wananchi wake.
Mahali pengine Mwalimu alinukuliwa akitetea Mapinduzi na kuwazodoa wenye hofu akisema: “Watu wanaoogopa Mapinduzi ni wanyonyaji; majitu yanakataa ‘Revolution’ ni manyonyaji, yamezoea ķunyonya. Msiyaogope!
“Mnyonge hawezi kusema mambo yaendelee vile vile, ila yale manyonyaji yaliyoshiba na yenye kuendelea kushiba kwa jasho la wanyonge.”
Utamaduni wa Mapinduzi ya kijeshi uliposimika mizizi Afrika miaka ya 1960 na hususan kufuatia kupinduliwa kwa Rais Kwame Nkrumah wa Ghana, Februari 24, 1966, Mwalimu alianza kuingiwa na hofu.
Mwathirika wa kwanza wa Mapinduzi ya kijeshi Afrika alikuwa Rais Sylivanus Epiphanio Olympio wa Togo, aliyeuawa Januari 13, 1963 na baadaye Nkrumah.
Hofu ya Mwalimu ni kwamba mambo yaliyosababisha Mapinduzj kipindi hicho yalikuwa yakitokea nchini mwake pia!
Yaani kuwapo kundi dogo linalojishibisha kwa jasho la wanyonge na kufunga mlango kwa komeo lisiguswe wakati likitapanya uchumi.
Mwaka 1966 Mwalimu aliwaita wakuu wa vyombo vya usalama; Jeshi la Ulinzi, Polisi, Usalama wa Taifa, Magereza na wengine, akawaambia: “Ninajua mmeyasikia (Mapinduzi ya kijeshi) yaliyotokea Ghana, na huenda nanyi mkashawishika kufanya hivyo hapa nyumbani. Kama mtapindua Serikali (yangu) pindueni mtakavyo ,lakini msimwage damu ya raia wangu.”
Kwa maneno hayo machache, akaondoka na kuwaacha midomo wazi, wakitazamana kwa mshangao bila kupata mantiki ya alichowaitia wala alichowaambia.
Serikali ya Nkrumah iliangushwa kwa sababu nyingi, kubwa kati ya hizo ni uchumi ķuendelea kuparaganyika, deni la nje kuongezeka na sababu kadhaa za ndani.
Miaka miwili nyuma, Januari 21, 1964, Jeshi la Tanganyika lilipoasi na kuzingira lkulu huku wanajeshi wakimtafuta Rais Nyerere aliyekuwemo ndani, Mwalimu hakutishika; badala yake alipandwa na ghadhabu akataka kutoka nje kwenda kukutana na waasi ili ‘awapashe’ kuhusu kitendo chao cha hovyo cha kuaibisha taifa.
Wasaidizi wake walifanya kazi ya ziada kumzuia asitoke, wakimweleza hatari ya kukutana na waasi wenye silaha. Mkewe, Maria Nyerere, akamsihi kwa kupiga magoti akilia kwa hofu. Maofisa usalama wakamshikilia Mwalimu huku akitweta kwa hasira.
Wakamtoroshea mafichoni, Kigamboni. Siku tano baadaye, akalihutubia taifa kutoka mafichoni na kulaani tukio hilo. Wakati huo waasi wameshadhibitiwa kwa msaada wa jeshi la Uingereza.
Askari wale waliasi kushinikiza maslahi bora na kuondolewa kwa maofisa wa kigeni jeshini nafasi zao zichukuliwe na wazalendo chini ya programu ya ‘Afrikanaizesheni’ iliyogusa karibu asilimia 95 ya taasisi za kiraia; isipokuwa Jeshi.
Kasi ya Mapinduzi ya kijeshi Afrika ilikuwa ya kutisha. Kati ya mwaka 1956 na mwishoni mwa 1985 wakati Mwalimu aking’atuka, kulitoke Mapinduzi ya kijeshi 60 yaliyofanikiwa. Wastani wa Mapinduzi mawili kila mwaka.
Mwaka 1966 pekee wakati Mwalimu alipowaeleza wakuu wa vyombo vya usalama namna bora ya kupindua seriķali, kulitokea Mapinduzi manane; kufikia mwaka 1986, kati ya nchi huru 50 za Kiafrika, ni 18 tu zilizokuwa chini ya utawala wa kiraia.
Maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) yalipotikisa utawala wakipinga wasomi kwenda Jeshi la Kuienga Taifa (JKT), Oktoba 1966, waķituhumu ķuibuka tabaka la ‘Wabenzi’ lililojinufaisha kwa matunda ya uhuru huku limefunga mlango kwa komeo kwa wanyonge, Mwalimu akayasoma maandiko ukutani.
Kwa kuguswa na maneno ya waandamanaji kwamba; “Afadhali Wakati wa Ukoloni kuliko enzi za Uhuru,” na uwezekano wa Serikali yake kuingia matatani kwa shinikizo la nguvu ya umma, ili kuepusha hilo, Februari 5, 1967 Mwalimu akatangaza Azimio la Arusha na Sera ya Ujamaa na Kujitegemea kuzuia kuzuka kwa matabaka na utegemezi kutoka nje.
Kwake, hiyo ilikuwa njia sahihi ya kusimamia Mapinduzi bila kuleta madhara kwa nchi badala ya ukaidi na ujuaji. Huo, kwa msamiati wa leo unaweza kuitwa uasi wenye kuambatana na uhaini.

Neema ya uasi kidini
Mwalimu angetuhumiwa kwa ‘ujadhambi’ kwa ķukandia au kozodoa viongozi wa dini, lakini haikuwa. Ni kwa sababu alielewa vyema nafasi na madhumuni ya dini kwa jamii hivi kwamba aligeuka kuwa kioo cha viongozi wa dini uchwara.
Mfano, hotuba yake kwenye Mkutano wa Shirika la Mary-Knoll, New York, Oktoba 1970 juu ya ‘Kanisa (dini) na Maisha ya Watu’, anashadidia uasi wa kidini kwa kuwazodoa viongozi wa ambao hujaribu kujitenga kando pale wale wanaoteseka kwa maonevu na umasikini wanapoanza kuchachamaa, kama binadamu, kujaribu kubadili hali.
“Kanisa likubali kuwa maendeleo ya watu maana yake ni maasi; (kwamba) katika historia watu hufikia hatua ya kuyakataa mambo yanayowabana kama binadamu.
“Ni jukumu la Kanisa (dini) kushiriki kwa vitendo katika mapambano ya kuondoa utaratibbu wa maisha na wa uchumi unaowadidimiza watu kwenye umasikini, uonevu na unyonge, bila hivyo Kanisa (dini) litakuwa halina uhusiano na maisha ya binadam, na dini itakuwa kama ni mkusanyiko wa imani za kishirikina zinazokubaliwa na wenye hofu tu. Kanisa (dini) litaambatanishwa na dhuluma na ujahili,” anasema Mwalimu.
Na ikiwa hivyo, anasema, Kanisa litakufa, kwani litakuwa halina maana inayoeleweka kwa mtu wa kisasa, na: “Maendeleo yawe na maana ya maasi matakatifu kwa lengo la kuleta mabadiliko. Lazima idhihirike kwamba Kanisa linashambulia waziwazi mtu au kikundi chochote kinachosaidia kudumisha unyonge huo wa mwili na roho, bila kujali misukosuko inayoweza kutokea kwa Kanisa au wafuasi wake; maana kiwa Kanisa halipingi maonevu yaliyoko, basi kuendelea kuwapo kwake na dini yote ya Kikristo, kutaambatanishwa na kuendelea kwa dhuluma.”
Anasema: “Kanisa litambue kwamba lina wajibu wa kuongoza Mapinduzi hayo kwa kushambulia shirika lolote, au utaratibu wowote wa uchumi, wa maisha ya watu, au wa siasa unaowakandamiza watu na unaowanyima haki na uwezo wa kuishi kama wana wa Mungu mwenye upendo.”
Hapa Mwalimu anatofautiana na Wahafidhina wa ubeberu wa ķiroho, na wanasiasa uchwara wanaodai kuwa, kufanya hivyo ni kuchanganya dini na siasa.
Kwa Mwalimu na wanaharakati wote wa haki za binadamu dhana ya kuchanganya dini na siasa ni uzandiki wenye lengo la kujenga taifa la ‘wateule’ na miungu watu kwa shinikizo kwa wenye haki kuacha wajibu wao wa kutetea wanyonge ili kujiepusha na kadhia ya waonevu wenye nguvu.
Hii ni kinyume cha mwasisi wa dini ya Kikristo, Yesu Kristo ambaye alitoa upinzani mkubwa dhidi ya watawala wadhalimu na ukandamizaii wa binadamu bila kujali kama watawala hao walikuwa ndugu au la, na kwa sababu hiyo akasema hakuja kuleta amani bali upanga (Luka 14:26).
Kwa Mwalimu, amani ni zao la haki, na kwamba bila haki hakuna amani. Anasema: “Huwezi kusema kwamba amani ipo kwa sababu hakuna vita; amani inayotegemea kupimana nguvu (kati ya waonevu na wenye ķuonewa) si amani. La!
“Amani ni kitu kinachokuzwa siku hadi siku kaika kuleta hali iliyokusudiwa, ambapo Mungu na msingi wake ni ukamilifu zaidi wa haki kati ya watu.”
Kwa kifupi, dini ni taasisi tata yenye kuhitaji ujasiri katika kuwakomboa watu kimwili na kiroho. Kiongozi wa kidini mwoga hapaswi kuwa sehemu ya mfumo wa dini, maana hawezi kuhubiri ukombozi wa kweli kwa wafuasi wake na kwa taifa kwa ujumla.
Je, siku ya kusulubiwa kwake, Kristo hakuwaambia wafuasi wake wauze kanzu zao wanunue mapanga? Na hiyo ndio dhamira ya uasi kwa watu wenye kuonewa, kukandamizwa na kunyimwa haki.
0713 526972