Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kagera

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Damas Ndumbaro amewataka wanasiasa kutojifanya hawayaoni maendeleo katika sekta mbalimbali yaliyoletwa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.

Dkt Ndumbaro ametoa wito huo katika nyakati mbalimbali akiwa ziarani Mkoani Kagera akikagua miradi ya maendeleo kama mlezi wa mkoa huo ili kujiridhisha endapo fedha zinazo tolewa na serikali zinatumika kwa ufanisi.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akipokea maelezo ya mwenendo wa utoaji wa huduma kutokwa kwa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Maruku wakati wa ziara yake hivi karibuni mkoani Kagera. Katika Ziara hiyo Waziri Ndumbaro aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Franklin Rwezimula pamoja na viongozi wengine wa Serikali na Chama (Picha na Wizara ya Katiba na Sheria)

Amesema,” hakuna asiyeona kazi kubwa aliyoifanya Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali, amejitahidi kugusa kila eneo iwe barabara,elimu, afya, ajira na sasa anahakikisha wananchi wake wanapata haki na kujua haki zao kupitia Kampeni ya Msaada wa kisheria inayo tekelezwa nchini kote”.

Amesisitiza kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wanatoa kauli za kupotosha kwa wananchi wakati serikali imefanya kazi kubwa katika sekta zote ili kuhakikisha nchi inapata maendeleo makubwa

Dkt Ndumbaro amekagua na kujiridhisha ubora katika miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mradi wa shule ya msingi Igayaza Wilayani Misenyi, mradi wa ujenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, ujenzi wa mradi wa maji Nyabiyonza wilayani Karagwe, ujenzi wa shule ya sekondari ya amali Katerero, zahanati ya Mulahya na mradi wa maji Kemondo wilayani Bukoba.

Miradi mingine aliyokagua Dkt Ndumbaro ni ujenzi wa sekondari ya kasheno na mradi wa maji Kamachumu-Bushagara wilayani Muleba pamoja na mradi ujenzi wa sekondari ya Kabindi na mradi wa maji Nyamigogo -songambele ya Wilayani Biharamulo.

Kwa upande wao viongozi mbalimbali mkoani Kagera wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kufanikisha ujenzi wa miradi mbalimbali.

Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo SACP Advera Bulimba amesema katika halmashauri ya Wilaya hiyo wamepokea shilingi bilioni 98 kutoka serikali kuu kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Julius Laizer amempongeza Rais Samia kwa kampeni ya Msaada wa Kisheria kwani inapunguza migogoro mingi ambayo imeshindikana kutokana na wananchi kukosa pesa za kugharamia wanasheria na mawakili.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (mwenye miwani) akiweka jiwe la Uzinduzi wa Mradi wa Maji Nyamigogo Songambele wakati wa ziara yake Mkoani Kagera.Katika Ziara hiyo Waziri Ndumbaro aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Franklin Rwezimula pamoja na viongozi wengine wa Serikali na Chama (Picha na Wizara ya Katiba na Sheria)