Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kinara katika ukanda wa Kusini mwa Afrika kwa kutoa fedha nyingi za ruzuku katika sekta ya kilimo cha mazao mbalimbali ya kibiashara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Benki ya Taifa ya Ushirika leo, Jumatatu Aprili 28, 2025, jijini Dodoma, Waziri Bashe alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali ya Rais Samia imetoa ruzuku ya takribani Shilingi bilioni 99.5 kwa ajili ya zao la pamba, sambamba na Shilingi bilioni 21 zilizotolewa kwa zao la tumbaku.
Aidha, Bashe alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imetoa jumla ya Shilingi bilioni 281 kwa ajili ya pembejeo na miche kwa mwaka wa fedha 2024/2025, hatua ambayo imewezesha wakulima kupatiwa pembejeo bure. Juhudi hizi zimechangia sekta ya korosho kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 520,000 — kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu Tanzania ipate uhuru.
Kutokana na mafanikio hayo, thamani ya mauzo ya mazao imefikia Shilingi trilioni 1.8 kwa mwaka 2024/2025, huku matarajio yakiwa kufikia kati ya Shilingi trilioni 1.8 hadi 1.9 ifikapo mwisho wa mwaka huu wa fedha.
Katika hatua nyingine, Waziri Bashe alielezea uwekezaji mkubwa wa Serikali katika ruzuku ya mbolea. Alibainisha kuwa mwaka 2021, wakati Rais Samia anahutubia Bunge, matumizi ya mbolea yalikuwa tani 360,000. Hadi kufikia mwaka 2023/2024, matumizi hayo yaliongezeka hadi tani 860,000, na kwa mwaka wa fedha 2024/2025 yanatarajiwa kufikia tani 1,200,000.
Kwa ujumla, Serikali imeshatoa Shilingi bilioni 653 kama ruzuku ya mbolea katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, hatua inayolenga kuimarisha uzalishaji na kuinua maisha ya wakulima nchini.

