Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga kutoa uamuzi wa hoja za Mawakili wa Jamhuri na Mawakili wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, Mei 6, 2025.
Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini baada ya kusikiliza hoja za kisheria baina ya upande wa Jamhuri na utetezi ambao uliwasilisha mapingamizi Mahakamani hapo tangu April 24, 2025 kuhusu mwenendo wa shauri hilo.
Kesi hiyo imesikilizwa leo kwa njia ya mtandao ambapo upande wa Jamhuri ulijibu hoja za Mawakili wa utetezi mbele ya Hakimu Mhini ambapo Lissu amegoma kushiriki tena kesi hiyo akiwa na msimamo wake wa kutaka afikishwe Mahakamani na si kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
Awali upande wa Jamhuri uliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutupilia mbali mapingamizi ya Mawakili wa utetezi katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu na miongoni mwa hoja za mapingamizi ya jopo la Mawakili wa utetezi takribani 31 wakiongozwa na Mpale Mpoki ni kwamba wanaiomba Mahakama hiyo itoe amri ya kuhojiwa kwa Afisa Magereza wa Mkoa na Mkuu wa Gereza la Ukonga kwamba kwanini Lissu hajafikishwa Mahakamani.
Baada ya kusikilizwa kwa hoja hizo, kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 6, 2025 kwa ajili ya kutolewa uamuzi.
