Waasi wa Kihouthi wa nchini Yemen wamesema shambulio la anga lililofanywa na Marekani lililokilenga kituo kinachowashikilia wahamiaji kutoka Afrika limewauwa watu 68. Kamandi kuu ya Marekani haijazungumzia tukio hilo.

Taarifa ya Wahouthi iliyotolewa mapema Jumatatu , imesema kando ya watu 68 waliouwawa katika shambulio hilo kwenye eneo la Saada, watu wengine 47 wamejeruhiwa. Kwa mujibu wa waasi hao wa Yemen  wahamiaji 115 walikuwa wakishikiliwa kwenye kituo hicho wakati wa shambulio hilo. Eneo lililoshambuliwa linafahamika kuwa ngome kubwa ya waasi hao.

Kituo cha televisheni cha Al Masirah chenye mfungamano na waasi wa Kihouthi kimeripoti kuwa shughuli za uokoaji na timu za huduma za dharura zinakabiliwa na changamoto kutokana na uharibifu mkubwa uliotokana na shambulio hilo. Picha za video zilizotolewa na kituo hicho zimeonesha kile kilichoonekana kuwa miili ya waliouwawa na watu waliojeruhiwa wakiwa katika eneo la tukio. Picha nyingine zilizotolewa  baadaye zimewaonesha majeruhi wakipatiwa matibabu hospitali.

Wizara ya mambo ya ndani iliyo chini ya serikali ya Wahouthi ambayo haitambuliwi kimataifa imelaani shambulio hilo iliyoliita kuwa”uhalifu wa kutisha uliofanywa na Marekani kwa kulenga kituo cha wahamiaji wasio na vibali kutoka Afrika”