Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamecharuka bungeni wakitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), liwe mamlaka ili iwe rahisi kuendesha shughuli zake.

Wabunge waliochangia makadirio ya bajeti ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira walisema jana kuwa kwa sasa NEMC ni kama kibogoyo na haina uwezo wa kuwachukulia hatua wanaoharibu mazingira.

Mbunge wa Sumve (CCM),Kasalali Emmanuel Mageni alisema NEMC kama chombo chenye dhamana ya Mazingira nchini kinatakiwa kusimamia mazingira kwa misingi ya Sheria na kutoa maamuzi yasiyoingiliwa wala kupingwa na mtu yeyote.

“Tukizungumzia suala la kelele, wananchi wamekuwa wakiteseka, mabaa yamejaa kila kona, bila kujali vibali vya maeneo husika, NEMC wakifungia, mamlaka nyingine zinakuja zinafungua, kwa hiyo inakuwa ni ngumu kusimamia utekelezaji wake”

Alisema mazingira yanaendelea kuharibiwa na shughuli za kibinadamu kutokana na kukosekana kwa mamlaka yenye nguvu ya kuchukua hatua kwa wanaoendelea kuharibu mazingira.

Mbunge mwingine, alisema ili iweze kufanya kazi zake kwa weledi lazima Sheria ifanyiwe marekebisho na kuwa Mamlaka kutoka kuwa Baraza ambalo alisema halina ngu ya kisheria.

Alitaja faida ya NEMC kuwa mamlaka kuwa ni pamoja na kuipa nguvu ya utekelezaji boraa wa sera mpya sheria na kanuni na kufanya maamuzi kwa urahisi kutekeleza vizuri matakwa ya Sheria na Kanuni na matumizi bora ya rasilimali fedha na rasilimali watu.

“Ndugu zangu mimi ni mjumbe wa kamati ya bajeti nafahamu namna ambavyo NEMC hawana fedha wala ubavu wa kutatua changamoto sasa ikiwa mamlaka kamili tutaiwezesha kutumia vyanzo vyake vya mapato virudi kwa wakazitumie,” alisema

“Huwezi ukawa ukanusanya faini zinazotokana na uhalibifu wa mazingira halafu haurudishi kufanya urejelezaji wa mazingira hatuwezi kwenda kwa namna hii,” alisema na kuongeza.

“NEMC ikiwa mamlaka tutaipa mtazamo wa kuaminika kwa umma na mataifa mengi yamefanikiwa kwasababu ya kuwa na mamlaka zinazosimamia mazingira, “ alisema

Aalitaja udhaifu wa sheria ya mwaka 1997 ambayo alisema haimtenganishi Waziri husika na utendaji wa kola siku wa NEMC hali inayosababisha mwingiliano wa majukumu.

“Unakuta waziri anadhamana ya kutoa vibali, kutoa leseni na vyeti, Wziri anatakiwa awe mamlaka ya rufaa kwamba NEMC wakitofautiana na wananchi wakate rufaa kwa waziri lakini siyo Waziri akate katikati ya utendaji,” alisema

“Mwaka 2021 tulifanya mapitio tukaunga sera mpya tofauti nay a 1997 kutokana na changamoto ya uhifadhi wa mazingira na tulikuwa tumeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa ya utunzaji wa mazingira ambayo ilitulazimu kutunga sera mpya imeelekeza baadhi ya mambo yafanyike,|

“Lakwanza kutazama mabadiliko ya tabia nchi, taka za kielektroniki, uchafuzi wa mazingira kutokana na uchimbaji wa mafuta na gesi na kemikali lakini haya yote tuliridhia lakini mpaka leo hatujayatungia sheria, hapa tunaweka rehani mazingira yetu” alisema.

“Ndiyo maana tunasimama hapa kusema tunataka tuwe na Mamlaka yenye dhamana ya kusimamia mazingira siyo baraza, Baraza liko kwa sheria ya zamani na majukumu yake hayaendani na changamoto za sasa za mazingira,” alisema

“Wakati tunatunga hii sheria mwaka 1997 haikugusia lolote kuhusu uchafuzi wa mazingira kwenye migodi lakini leo hii tuna migodi mingi sana na athari za mazingira zimekuwa nyingi kwa hiyo tutunge sheria ambayo itaendana na sera ya mwaka 2021 na Sheria ambayo itaifanya NEMC kuwa mamlaka kamili,”alisema

Awali akiwasilisha hotuba ya mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/205 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/2026 Mhandisi Hamad Masauni, alisema Baraza litaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, sura 191 kwa kuendelea kutekeleza sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021.

Alisema NEMC itaendelea kutekeleza mkakati wa Taifa wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034), kuendelea kuratibu mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira, kusajili wataalam elekezi wa Mazingira na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya hifadhi na usimamizi wa mazingira.