Na Lookman Miraji


Siku ya mfalme ni siku maarufu sana nchini Uholanzi. Siku hiyo ya wafalme hujulikana kwa jina la “Koningsday” kwa lugha ya kiholanzi na “King’s Day” kwa tafsiri ya lugha ya kiingereza.


Siku hii ya wafalme hutambulika kama siku ya sherehe za kitaifa inayoadhimishwa kwa heshima ya mfalme wa Uholanzi.


Historia ya siku hii ilianza kusheherekewa katika karne ya 19 kuanzia mwaka 1885 ikitambulika kama siku ya malkia Wilhelmina ambaye alikuwa malkia wa Uholanzi wakati huo.


Kwa wakati huo siku hii ilikuwa ikiadhimishwa kwa lengo la la kuimarisha mshikamano wa kitaifa ambapo maadhimisho yake yalikuwa yakifanyika kila tarehe ya kuzaliwa kwa malkia aliye madarakani.


Historia ya siku hii imekuwa ikipita katika mabadiliko ya tarehe kulingana na watawala waliowahi kupita katika madarakani ya kuliongoza taifa hilo.


Tukirejea katika historia ya taifa la Uholanzi, katika uongozi wa malkia Juliana ambae mabadiliko ya siku hiyo ilipitishwa kuadhimishwa katika siku yake ya kuzaliwa ambayo ilikuwa ni Aprili 30 ndipo siku hiyo ilipofanywa kuwa “Koninginnedag” rasmi yaani siku ya malkia.


Tarehe 30 ya mwezi Aprili ilibaki kuwa sikukuu ya kitaifa nchini humo mpaka katika 1980 pale alipoingia madarakani malkia Beatrix.

Hata hivyo mtawala huyo alipoingia madarakani kwa wakati huo hakubadili tarehe ya siku hiyo licha ya kwamba yeye alizaliwa mwezi Januari sababu ikitajwa kuwa hali ya hewa ya mwezi Aprili ni nzuri zaidi kwa sherehe za nnje. Pia ikumbukwe malkia Beatrix ni mtoto wa malkia Juliana aliyemtangulia


KUTOKA SIKU MALKIA MPAKA SIKU YA MFALME.


Mabadiliko ya siku hii kutoka kuwa siku ya malkia mpaka kuwa siku ya mfalme yalichagizwa na mabadiliko ya muundo wa kiutawala, kwani uongozi ulibadilika mwaka 2013 ambapo malkia Beatrix alijiuzulu na nafasi yake kurithiwa na mfalme Willem Alexander. Hapo ndipo jina la siku hiyo ikabadilika na kuwa siku ya mfalme.


Tangu wakati huo siku hiyo pia ikafanyiwa mabadiliko ya tarehe na kuanza kusheherekewa katika tarehe 27 mwezi Aprili ikiwa ni siku ya kuzaliwa ya mfalme Willem.


Mfalme Willem Alexander alizaliwa Aprili 27, mwaka 1967 huko Utrecht nchini Uholanzi akiwa mtoto wa kwanza wa malkia Beatrix na Prince Claus. Mwaka 2013 baada ya malkia Beatrix kustaafu Willem alitawazwa kuwa mfalme mpya wa taifa hilo na kuweka rekodi ya kuwa mwanaume wa kwanza kushika nafasi hiyo ya juu zaidi tangu mwaka 1890.


MATUKIO YANAYOFANYIKA KATIKA SHEREHE ZA SIKU YA MFALME


Sherehe hizo za siku ya mfalme nchini Uholanzi ni mchanganyiko wa mila za kifalme na furaha ya kitaifa ambapo miji yote hujawa na burudani, biashara katika masoko ya wazi, gwaride na watu waliovaa rangi ya machungwa ikiwa ni ishara ya familia ya kifalme “House of Orange”.


Wageni na wenyeji nchini humo hushiriki kwa furaha huku mitaa mingi ikijawa na burudani. Hakika endapo ukiwa Uholanzi wakati wa siku ya mfalme “Koningsday” ni mojawapo ya sherehe za kitaifa zenye furaha zaidi, rangi na ushirikiano mkubwa wa jamii.

Hivyo hivyo pia kwa hapa nchini Tanzania, kupitia ubalozi wa Uholanzi hapa nchini imeadhimisha siku hiyo ikiwa ni sehemu ya kuendelea kudumisha tamaduni za sherehe za siku hiyo. Maadhimisho hayo ya siku ya mfalme yaliongozwa na balozi wa Ufalme wa Uholanzi nchini, Wiebe de Boer.

Waziri wa mambo ya nnje ya nchi, Balozi Mahmoud Thabit Kombo alishiriki akiwa kama mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku hiyo ya kuzaliwa kwa mfalme wa Uholanzi iliyofanyika katika makazi rasmi ya Balozi wa Uholanzi, jijjni Dar es salaam, Aprili 24 2025.

Balozi Kombo akiwa kama mgeni rasmi katika shughuli hiyo ameishukuru serikali ya Uholanzi kwa mchango wake katika maendeleo ya watanzania kupitia sekta za kilimo, afya, mani, elimu, utalii na uwekezaji ambapo aliahidi kukuza uhusiano na urafiki kwaajili ya manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

“Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Uholanzi umejengwa kutokana na historia ya ushirikiano wa kirafiki ulioasisiwa na Mfalme Bernhard wa Lippe-Biesterfield na hayati Julius Nyerere. Maadili waliyoamini pamoja yamekuwa msingi wa ushirikiano thabiti na wenye manufaa tunaouendeleza hadi leo”. Alisema Waziri Kombo.

Aidha pia Balozi wa Uholanzi nchini, Wiebe de Boer, ameishukuru serikali ya Tanzania kwa heshima ya ushiriki wake katika maadhimisho ya siku hiyo huku akiahidi kudumisha uhusiano huo uliopo.

“Uholanzi ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa wa kigeni nchini Tanzania. Ikiwa na zaidi ya kampuni 100 za kiholanzi zilizowekeza zaidi ya euro milioni 300 na kuunda ajira zipatazo 27000 jambo linadhihirisha dhamira ya Uholanzi katika uchumi wa Tanzania”. Alisema balozi huyo.

Mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Uholanzi yamekuwa yakidumu kwa zaidi ya miongo mitano tangu yalipoasisiwa rasmi mwaka 1970.