Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mbeya
CHAMA cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu nchini (THRDC) wamelaani kuanza kuibuka matukio ya waandishi wa habari na watangazaji kukamatwa na baadhi kupigwa na hata kuharibiwa vifaa vyao vya kazi na vyombo vya dola.
Kauli ya kulaani imetolewa leo Aprili 25 mwaka huu na Mwenyekiti wa JOWUTA Mussa Juma leo mkoani Mbeya, wakati wa mafunzo kwa wanahabari kuhusu uandishi wa habari za uchaguzi, ulinzi na usalama kazini.
Mafunzo hayo yamehusisha waandishi kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe, ambapo Juma amesema matukio ya kukamatwa, kupigwa na kuharibiwa vitendea kazi hayakubaliki katika nchi inayojinadi kuwa inazingatia misingi ya kidemokrasia.

Juma amesema katika siku za karibuni, kumeanza kutokea matukio ya baadhi ya wanahabari kukamatwa na vyombo vya dola, kupigwa na wengine kuzuiwa kufanyakazi, jambo ambalo sio sahihi.
Mwenyekiti huyo, amesema mahusiano mazuri baina ya vyombo vya dola na wanahabari, yalikuwa yameimarishwa katika siku za nyuma lakini sasa yanaanza kuharibika jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa.
“Kama mwanahabari amekiuka taratibu zozote kuna utaratibu wa kufuata kisheria, badala ya kutumika nguvu kumkamata ama kumzuia kufanyakazi yake”amesema.

Hata hivyo, Juma amewataka wanahabari nchini, kufanyakazi kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa Habari, hasa kipindi hiki cha harakati za uchaguzi mkuu, ikiwepo kutoandika habari za upendeleo kwa chama chochote za siasa, kuacha kuwa washabiki wa vyama na watowe fursa sawa kwa vyama vyote.
“Msimamo wa JOWUTA kama mwanahabari unataka kujihusisha na masuala ya siasa ni bora kujiweka kando mapema na tasnia ya habari hadi chaguzi zipite, badala ya kutumia chombo chako cha habari kwa maslahi binafsi ya kisiasa”amesema.
Awali,Wakili Jones Sendodo wa kutoka THRDC, amesema mtandao huo unaungana na wadau wote kulaani matukio yoyote ya kunyanyaswa, kupigwa ama kuharibiwa vitendea kazi mtetezi wa haki za binaadamu, wakiwepo wanahabari.
Wakili Sendodo amesema ni vyema vyombo vya dola kuzingatia sheria za nchi wakati wa kutekeleza wajibu wao.

“Tunapinga matukio ambayo yanaendelea kwa vyombo vya dola kutumia nguvu kubwa kuwanyanyasa watetezi wa haki za binaadamu na sisi kama THRDC kwa kushirikiana na wadau wengine tutaendelea kuwatetea na kuwapa msaada wa kisheria, msaada wa ushauri wa kisaikolojia na hata makazi salama ya muda watetezi wa haki za binaadamu wakiwepo wanahabari wanapokabiliwa na majanga ama vitisho”amesema.
Wakili Sendodo pia akitoa mada katika mafunzo hayo ya uchaguzi kwa wanahabari, aliwataka kujua sheria mbalimbali ambazo zinawahusu ili kujitahidi kutozivunja, ikiwepo Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016, Sheria ya Takwimu, Sheria za Uchaguzi na nyingine.
Hata hivyo, alitaka wanahabari kujali usalama wao wakiwa kazini na kuchukuwa tahadhari mbali mbali ili kuhakikisha wakati wote wanabaki salama, wakati wakitekeleza wajibu wao.
Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya aliwataka wanahabari nchini, kuendelea kujiunga na JOWUTA kwani ndio chama pekee kinachotambulika kisheria kutetea maslahi ya wafanyakazi katika vyombo vya habari na mazingira bora ya kazi.
“Tumekuja kuwapa elimu ya uchaguzi, lakini pia nitumie nafasi hii kuwaomba wafanyakazi wa vyombo vya habari mjiunge JOWUTA, ili tuwe na nguvu moja ya kupigania maslahi yetu,” amesema.
JOWUTA inaendelea na kutoa mafunzo kwa wanahabari nchini kuhusiana na kuripoti vyema uchaguzi mkuu mwaka huu na kubaki salama, mafunzo hayo yamedhaminiwa na Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari (IFJ), Shirikisho la Waandishi wa Habari Afrika (FAJ),THRDC, Taasisi wa Wanahabari ya Kusaidia Jamii za Pembezoni (MAIPAC) na JOWUTA.

