Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali imewasilisha mbele ya Bunge vipaumbele vitano vya Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) kwa mwaka wa fedha 2025/26 vinavyolenga kuongeza ufanisi wa taasisi za umma, usimamizi wa rasilimali za umma na kukuza mapato yasiyo ya kodi.

Vipaumbele hivyo viliwasilishwa Alhamisi, Aprili 24, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo alipokuwa anawasilisha mapendekezo ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha utakaoanza Julai 1, 2025, ambapo ameomba kuidhinishiwa Sh148.63 bilioni kwaajili ya kutekeleza shughuli na vipaumbele mbalimbali.

Miongoni mwa maeneo ya vipaumbele kwa upande wa OMH ni utekelezaji wa Mpango wa Muda Mrefu wa miaka 25, unaotarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2025/26 hadi mwaka 2049/50.

Mpango huu utatoa mwongozo wa muda mrefu kuhusu maeneo ya uwekezaji, usimamizi wa mali za serikali na mwelekeo wa kiuchumi unaoendana na dira ya taifa.

Aidha, Mhe. Waziri Mkumbo alisema serikali itaendelea kufanya tathmini na ufuatiliaji wa mali za serikali zilizopo chini ya usimamizi wa OMH pamoja na zile zilizobinafsishwa, ikiwemo mashamba, viwanda, nyumba na viwanja.

“Lengo la serikali ni kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali hizo kwa manufaa ya umma,” alisema.

Katika kuongeza ufanisi, Serikali imepanga kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuuongeza ufanisi wa OMH katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kikodi.

OMH iko kwenye mchakato wa kufanya maboresho makubwa kwenye matumizi ya TEHAMA kwa kuandaa Dash bodi ambayo itarahisisha utekelezaji wa majukumu.

Maboresho hayo yatawezesha upatikanaji wa takwimu kwa wakati, kuongeza uwazi na kurahisisha usimamizi wa mapato yasiyo ya kodi.


Kutokana na umuhimu wake, mashirika ya umma yamehimizwa kutenga bajeti kwaajili ya kuwekeza kwenye mifumo ya TEHAMA inayosomana.

Ofisi pia kwa mwaka wa fedha ujao, itajikita kwenye kuboresha usimamizi wa taasisi na mashirika ya umma, kampuni tanzu na zile ambazo serikali ni mbia.

Hili linajumuisha matumizi ya miongozo maalum kuhusu majukumu ya wajumbe wa bodi, tathmini ya utendaji kazi na nafasi ya wawakilishi wa Serikali katika taasisi zenye umiliki wa hisa chache.

Miongozo hiyo ni pamoja na Waraka wa Msajili wa Hazina Na. 1 wa mwaka 2023, Mwongozo wa Majukumu na Matarajio ya Serikali kwa Wajumbe wa Bodi, Mwongozo wa tathmini ya utendaji kazi wa Bodi za Wakurugenzi na Mwongozo wa Wawakilishi wa Serikali kwa Taasisi ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache.

OMH pia itajikita kwenye kuimarisha uwezo wa kiutendaji kwa watumishi wake, kwa kuwajengea uwezo ili kuongeza tija na ufanisi wa kazi zao.


Kwa upande wa mapato, Serikali kupitia OMH imepanga kukusanya Sh1.56 trilioni katika mwaka wa fedha 2025/26.

Mapato hayo yatatokana na vyanzo visivyo vya kodi kama gawio kutoka mashirika ya umma, michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi, mapato kupitia mfumo wa TTMS, pamoja na rejesho la mikopo, riba na mapato mengineyo.

Kiasi hiki ni ongezeko kutoka Sh1.113 trilioni zilizoidhinishwa katika mwaka wa fedha unaoishia, yaani 2024/25.

Hadi kufikia Machi 2025, jumla ya Sh664.53 bilioni zilikuwa zimekusanywa, sawa na asilimia 60 ya lengo la mwaka mzima na asilimia 86 ya lengo la kipindi hicho.

Mafanikio haya yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na hatua ya Serikali kuimarisha mifumo ya TEHAMA kwa kuunganisha mifumo muhimu kama PlanRep, ERMS, e-Watumishi, na kuboresha mfumo wa MUSE.

Mhe. Prof. Mkumbo alisema maboresho haya yamewezesha upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu mapato na matumizi ya taasisi za umma, hivyo kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa fedha za umma.

“Tuna imani kuwa lengo la mwaka wa fedha 2024/25 la kukusanya Sh1.113 trilioni litatimia kwani sehemu kubwa ya makusanyo itapatikana katika kipindi cha robo ya nne ya mwaka,” alisema wakati akiwasilisha taarifa hiyo bungeni.