Rais Jakaya Kikwete mwishoni mwa wiki wakati akitoa tuzo za wanahabari bora nchini, ameviomba vyombo vya habari kuhakikisha vinatumia vyema uhuru wa habari katika mchakato wa Katiba mpya, aliotangaza rasmi kuwa utaanza hivi karibuni.
Rais Kikwete amesema si muda mrefu ataunda Tume ya Marekebisho ya Katiba, lakini akasisitiza: “Nawaomba wanahabari mhakikishe kuwa mchakato huu hauleti joto la kuigawa nchi. Nchi pekee tuliyonayo hapa kwetu ni hii. Hatuna Tanzania nyingine, ni yetu sote.”
Hatua ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kwamba Tume ya Kupitia Mapendekezo ya Katiba itaundwa April, imepongezwa kuwa ni hatua muhimu kuelekea kuyakabili masuala yanayotatanisha kikatiba nchini Tanzania.
Mchakato wa kuiandika upya Katiba ya Tanzania utatoa nafasi ya kuyatatua mambo mengi yenye migogoro, alisema Deus Kibamba, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, linalojumuisha Asasi za Kiraia zenye nia ya kukuza demokrasia nchini kwa kuzihusisha jamii zipatazo 180.
“Rais ametangaza hadharani kwamba mwezi ujao (Aprili) ataunda Tume ya Kutunga Katiba Mpya, ambayo itakusanya maoni ya Watanzania kutoka kada mbalimbali… huu ndiyo wakati tuliokuwa tukiusubiri, na taifa ndiyo linaanza mchakato wa kuzaliwa upya,” Kibamba aliiambia JAMHURI wiki iliyopita.
Kuandika Katiba mpya ni jambo lililoleta mkinzano mkubwa nchini Tanzania, hasa kuhusiana na jukumu la Serikali kuu na yale ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Katiba mpya inatarajiwa kuifufuwa Serikali ya Tanganyika, kuwapo sambamba na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mwaka 1964, Tanganyika iliungana na Zanzibar na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya Muungano huo, Serikali ya Tanganyika ilimezwa ndani ya Serikali ya Muungano, lakini ile ya Zanzibar iliendelea kufanya kazi.
Chini ya Katiba ya sasa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina nusu ya mamlaka na utawala juu ya mambo yote isipokuwa mambo 22 ya Muungano yanayojumuisha fedha, mambo ya nje, ulinzi na usalama, kutangazwa kwa hali ya hatari, uhamiaji na madeni ya kitaifa na biashara na mengine.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaunga mkono mfumo uliopo wa Muungano, lakini karibu vyama vyote vya upinzani vinataka kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika.
“Wananchi wana haki ya kuamua aidha kuunga mkono sera yetu ya serikali mbili au sera ya upinzani inayodai serikali tatu,” Katibu wa CCM wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amekaririwa akisema hivi karibuni na kuongeza:
“Lakini sababu zetu ziko wazi juu ya hili. Gharama kubwa kuwa na serikali tatu, (hivyo) ni bora kuendelea na mfumo uliopo wa serikali mbili.”
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, aliiambia JAMHURI kwamba wakati wa kufanya marekebisho ya katiba na kuruhusu serikali tatu umewadia, na kwamba hiyo ndiyo njia pekee ya kurejesha matumaini kwa taifa na kusaidia kukuza uchumi.
Zitto alisema kuwa Chadema itapigia kampeni kurudishwa kwa Serikali ya Tanganyika
Kwa mujibu wa Mwanasheria wa Mambo ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi, mambo ya ziada yanayopaswa kuongezwa katika Katiba mpya ni mgawanyo wa madaraka, kupunguza mamlaka ya Rais, haki ya kupata elimu na matibabu na haki ya kupata habari.
Chini ya mfumo uliopo, Kibamba alisema, Rais ndiye pia mwenyekiti wa chama tawala na anaongoza mikutano ya chama ikiwamo ile ya kumteua mgombea Uspika wa Bunge. Rais huteua pia Jaji Mkuu na majaji, wakuu wa mikoa na wilaya.
Kibamba anataka haki ya kupata elimu na matibabu ipewe uzito wa kisheria kama ilivyo haki ya kuishi.
“Hata kama mtu atatishia kukuua, Katiba inasimama kukulinda. Tunataka nguvu hizo hizo zifanye kazi kwa elimu na afya kwa raia wa Tanzania,” alisema Kibamba.
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mkoba, aliiambia JAMHURI kuwa walimu wanaunda asilimia 56 ya waajiriwa wa Serikali, lakini bado ajira yao inasimamiwa na idara tano tofauti, hivyo kuleta ugumu na kuondoa ufanisi.
Anasema chama chake kinapigania kuwa na kipengele katika Katiba, kitakachoanzisha Tume ya Huduma za Walimu kama ilivyo nchini Kenya.
Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga, anasema katiba iliyopo sasa inatoa miongozo ya haki ya kutoa habari, lakini inashindwa kutoa dhamana kwa uhuru wa vyombo vya habari.
MCT imeunda Kamati ya watu watano kuandaa kifungu maalumu cha Uhuru wa Vyombo vya Habari, kitakachowasilishwa katika Tume ya Katiba ili kiweze kuingizwa.
Rais Kikwete amesema Katiba mpya itakuwa tayari ifikapo mwaka 2014 na itakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kenya imewachukua miaka saba kuandika Katiba mpya.