Takriban watu tisa wameuawa na wengine 60 kujeruhiwa, wakiwemo watoto, katika shambulio la usiku la kombora la Urusi na ndege zisizo na rubani kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, amesema afisa wa eneo hilo.
Meya wa Kyiv, Vitali Klitschko amesema mabaki ya droni iliyoanguaka imesababisha moto, na kuna hofu kwamba watu kadhaa wamenasa chini ya vifusi vya jengo la makazi lililoharibiwa.
Milipuko pia iliripotiwa katika mji wa kaskazini-mashariki wa Kharkiv. Takriban watu wawili walijeruhiwa huko, amesema Meya.
Haya yanajiri saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kumshutumu Volodymyr Zelensky kwa kuharibu mazungumzo ya amani, baada ya rais wa Ukraine kukataa kutambua udhibiti wa Urusi wa eneo la Crimea.
Ukraine imerudia kusema haitaiacha Crimea, peninsula ya kusini iliyonyakuliwa kinyume cha sheria na Urusi mwaka 2014.
Rais wa Urusi Vladimir Putin alifanya uvamizi dhidi ya Ukraine mwaka 2022, na Moscow kwa sasa inadhibiti karibu asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine.
