Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kesi ya inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amegoma kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
Ulinzi mkali umeimarishwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, hususani katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kufuatia kusikilizwa kwa kesi inayomkabili Tundu Lissu.
Waandishi wa habari na wafuasi wa CHADEMA wamezuiwa kusogea karibu na jengo la mahakama.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka CHADEMA, baadhi ya viongozi wa chama hicho waliokuwa wakielekea kusikiliza kesi hiyo wamekamatwa, akiwemo Makamu Mwenyekiti John Heche na Katibu Mkuu John Mnyika.
Jeshi la Polisi limeendelea kutoa onyo kwa wanachama wa CHADEMA nchini kote, likiwataka kuepuka mikusanyiko isiyo rasmi.
Sababu za Kugoma
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alieleza kuwa sheria iko wazi kuhusu umuhimu wa mshtakiwa kuwepo mahakamani wakati wa kusomewa hoja za awali. Alisisitiza kuwa Lissu anapaswa kufikishwa mahakamani ili kuhakikisha haki zake za kikatiba zinalindwa.
Kwa upande wa mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema, alieleza kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali na upande wa mashtaka upo tayari, ila mshtakiwa hayupo mahakamani.
Hata hivyo, askari wa Magereza aliyekuwa ameunganishwa kwa njia ya video alieleza kuwa Lissu alikataa kusikiliza kesi kwa njia ya mtandao, akisisitiza kuwa anataka kesi hiyo isikilizwe kwa njia ya wazi.
Ulinzi mkali mahakamani
Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wamedhibiti eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo umati wa wanachama na wafuasi wa CHADEMA walifika kufuatilia kesi hiyo.
Polisi wenye silaha, mbwa na farasi walionekana wakiimarisha ulinzi tangu alfajiri hadi saa tatu asubuhi wakati kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
