Rais Samia apongezwa kwa mageuzi makubwa ya sekta ya madini
Wizara yafikia lengo kabla ya mwaka 2025
*Mavunde awashukuru watendaji, watumishi na wadau *
NA Mwandishi Wetu, JakhuriMedia, Dodoma
Wizara ya Madini imetangaza kuwa Sekta ya Madini hapa nchini imepiga hatua kubwa ya kihistoria kwa kufikia mchango wa asilimia 10.1 katika Pato la Taifa kwa mwaka 2024, ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya lengo lililowekwa katika Sera ya Madini ya mwaka 2009 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026).
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alipozungumza Dodoma leo na kueleza kuwa mafanikio hayo makubwa yametokana na usimamizi na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na uongozi wake mahiri uliosababisha sekta hiyo kufikia hatua hiyo muhimu mapema zaidi ya matarajio.

“Ni jambo la kujivunia kuona kuwa juhudi za serikali na wadau wa sekta hii zimezaa matunda. Mwaka 2023 tulikuwa na mchango wa asilimia 9.1 kwenye Pato la Taifa. Leo hii, tunazungumza kuhusu ongezeko hadi asilimia 10.1 kwa mwaka 2024. Hili si jambo dogo,” amesema.
Mavunde amesema mafanikio hayo yametokana na mabadiliko makubwa ya kimfumo na kisheria yaliyofanyika katika Sekta ya Madini tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Sita.
Amezitaja hatua zilizochangia mafanikio hayo kuwa ni kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli ya serikali kupitia sekta hiyo, kuanzishwa kwa minada ya madini ya vito, udhibiti wa utoroshwaji wa madini, kuanzishwa kwa masoko na vituo vya ununuzi wa madini pamoja na kuanza kwa ununuzi wa dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Aidha, amewashukuru wadau wote wa sekta ya madini wakiwamo wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo pamoja na wahusika wote waliopo katima mnyororo mzima wa sekta ya madini, watendaji wote wa sekta na taasisi zake kwa ushirikiano mzuri na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.

Vilevile, amewataka wawekezaji wote kuendelea kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa chini ya Sheria ya Madini, Sura ya 123, huku wizara ikiendelea kutoa ushirikiano kwa wote wenye nia ya kuwekeza kwa tija.
Pia amesena mafanikio hayo yameonesha wazi kuwa Sekta ya Madini si tu kichocheo cha ukuaji wa uchumi bali pia ni chanzo kikuu cha fedha za kigeni, ajira, na maendeleo ya kijamii kwa Watanzania.





