Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wadau wa utalii wa vyakula kuwekeza zaidi katika kuandika vitabu vya vyakula vya Kiafrika na machapisho ya kuandaa mapishi ili kuongeza ujuzi na kupunguza woga kwa watalii wa matumizi ya vyakula wasivyovifahamu.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa wa Utalii wa Vyakula Barani Afrika unaofanyika katika Ukumbi wa Gran Melia Jijini Arusha. Amesema ni muhimu kutangaza kwa kiwango kikubwa vyakula vya kitamaduni vya Afrika ili utalii wa vyakula uweze kukua na kustawi. Ameongeza kwamba kwa sasa watalii wengi hawana ufahamu wa utajiri wa Vyakula vya Kitamaduni vilivyopo Barani Afrika, vilevile ndani ya nchi za Afrika, utalii wa vyakula umewekwa kwa kiwango kidogo katika mikakati ya kitaifa ya maendeleo ya utalii.

Aidha Makamu wa Rais amesema katika kukuza utalii wa vyakula Barani Afrika inahitajika utengaji wa maeneo maalum na njia za kitamaduni ambapo bidhaa za ndani na vyakula vya kipekee vitatayarishwa kwaajili ya watalii kufurahia. Amesema katika njia na vituo hivyo vya chakula, ubora wa vyakula na bidhaa za asili ni lazima kudumishwa. Ameongeza kwamba hivyo kunahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wapishi wa vyakula vya asili, wazalishaji wa ndani, waongozaji watalii na wadau wengine wa utalii ili kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa kwa watalii ni endelevu.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema ipo haja ya kuweka utalii wa vyakula katika msingi wa utambulisho wa utalii wa Afrika ikiwemo kuimarisha mvuto wake kimataifa kwa kuweka mikakati ya kuunganisha uzalishaji wa chakula, uzoefu wa upishi, na huduma za utalii ili kuwa na athari endelevu za ndani za kiuchumi. vyakula vyetu tajiri, kupika na kula kwa ulimwengu.

Kwa upande wa juhudi za ndani ya nchi, Makamu wa Rais amesema katika kuhakikisha kunakuwepo na utalii endelevu wa vyakula, Serikali ya Tanzania imeamua kuimarisha ushirikiano na wazalishaji wa ndani wa kilimo ili kutekeleza mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuwekeza katika mifumo ya kidijitali inayowezesha uhusiano kati ya watalii, soko pamoja na na wazalishaji halisi wa chakula.

Makamu wa Rais amesema utalii wa vyakula una uwezo wa kuboresha hali ya lishe kwa kuwa unatoa mwongozo wa kuandaa chakula ambacho kinavutia na kinachoendana na utamaduni, huku ikihakikisha kuwa vyakula hivyo vinasaidia afya na ustawi. Amesema ni muhimu kubadilisha mwelekeo wa kitamaduni wa ladha na uwasilishaji wa chakula kwa afya na uendelevu katika kuoanisha uzuri wa chakula  na ufahamu wa afya.

Pia amesema Utalii wa Vyakula una nafasi ya kipekee katika sekta ya utalii na uwezo mkubwa wa kuchochea ukuaji wa uchumi shirikishi kupitia mchanganyiko wa bidhaa za utalii na kuwezesha jamii za wenyeji. Ameongeza kwamba Utalii wa chakula ni chombo muhimu cha kulinda urithi wa kitamaduni wa Bara la Afrika.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Utalii wa Chakula una nafasi kubwa ya kuvutia watalii Barani Afrika kwa kuwa nchi hizo zimejaaliwa kuwa na mazao mbalimbali, viungo na ladha za kipekee.

Ameongeza kwamba katika kusherehekea umuhimu wa vyakula katika nyanja ya utalii, ni muhimu kuwa na mpango endelevu na jumuishi ikiwemo kuwawezesha wakulima wa ndani, wapishi na wajasiriamali wa chakula kuwa sehemu ya mpango huo. Pia kuchagiza mpango wa mazao ya kutoka shambani hadi mezani ambao huongeza uzalishaji wa chakula wa ndani huku ukipunguza athari za mazingira pamoja na kuimarisha usalama wa chakula na viwango vya ubora ili kuweka imani katika bidhaa za vyakula.

Awali akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya Tamasha la Utalii wa Chakula, Mwanzilishi wa Tamasha hilo ambaye ni Mwenza wa Rais wa Zimbabwe Dkt. Auxilia  Mnangagwa  amesema kimataifa utalii wa chakula unafahamika kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi na uwezeshaji wa kijamii pamoja na kama njia ya kuondoa umasikini.

Amesema utalii wa chakula unawezesha kutengeneza ajira na upataji kipato pamoja na kuimarisha mikakati ya ushirikiano ambayo hupelekea kuwepo na mnyororo wa thamani wa kutegemeana kiuchumi katika jamii. Pia ni msingi wa ukuaji jumuishi ambao unatoa nafasi ya kipekee katika kuchochea maendeleo endelevu, kulinda tamaduni na kuwezesha jamii za asili ndani ya bara la Afrika.

Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa wa Utalii wa Vyakula Barani Afrika unafanyika kwa siku tatu Jijini Arusha ukishirikisha wadau mbalimbali wa vyakula kutoka ndani na nje ya bara la Afrika kwa lengo la kuhamasisha fursa zilizopo katika Utalii wa Vyakula kwa maendeleo endelevu.