Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Namtumbo
Wananchi wa vijiji vya Magazini, Sasawala, Amani na Likusanguse wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wameishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuwaletea gari la kubebea wagonjwa katika kituo cha afya cha Magazini kilichopo umbali wa zaidi ya kilomita 230 kutoka makao makuu ya Kata ya Magazini hadi Makao Makuu ya Wilaya ya Namtumbo ambako kuna hospitali ya Serikali ya Wilaya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari kwenye hafla ya kukabidhi gari la kubebea wagonjwa ambalo Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa amelikabidhi kwa wananchi wa kata hiyo wamesema kuwa gari hilo litawasaidia kuokoa maisha ya watu kwa kuwapeleka hospitali kubwa pale inapobidi tofauti na awali wagonjwa walikuwa wakisafirishwa kwa kutumia matenga, baiskeli na pikipiki.

Anold Mbunda Mkazi wa kijiji cha Lingusenguse alisema kuwa walikuwa wanapata adha kubwa kwa wamama wajawazito wanapotaka kwenda hospitali kubwa kwa ajili ya kujifungua wanatembea umbali mrefu zaidi ya kilomita 230 ambako kuna Hospitali ya Serikali.
Ambros January Jungu (Kaduguda) mkazi wa Kijiji cha Magazine alisema kuwa anamshukuru Mbunge Vita Kawawa pamoja na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwani kwa muda mrefu wananchi wa kata ya Magazini wakiwemo akina mama walikuwa wakisafirishwa kwenye Matenga walikuwa wakidhalilika wakati wanafuata huduma ya matibabu lakini leo wamepata gari ya kubebea wagonjwa litawasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa kero zilizokuwa zinawakabili apo awali.
Naye Tizo Matembo mkazi wa kijiji cha magazini alisema wanaishukuru Serikali kwa kuwapatia gari la kubebea wagonjwa kwani tokea mwanzo walikuwa na matatizo ya usafiri wagonjwa wengi walikuwa wanafia njiani kabla ya kufikishwa hospilati ya wilaya kutoakana na umbali mrefu na walikuwa wanatumia usafiri wa baiskeli.
Kwa upande wake Tabia Nguche muhudumu wa afya ngazi ya jamii kituo cha Magazini alisema kuwa awali walikuwa wakipata usumbufu mkubwa hivyo kitendo cha serikali kuwaletea gari la kubebea wagonjwa wakazi wa kata ya Magazini itapunguza changamoto ya muda mrefu ambayo ilikuwa ni kero hasa kwa akina mama wajawazito wanaotaka kujifungua ambao baadhi yao walikuwa wakijifungulia njiani wakati wakisafirishwa kwa matenga kwenda hospitali ya Wilaya.
Thabiti Shaibu Nnambi chifu wa kabila la Wayao eneo la Magazini alisema kuwa hivi karibuni wamepoteza watu zaidi ya kumi kupitia kuwabeba wagonjwa kwa kutumia matenga kichwani hivyo wanamshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassani pamoja na Mbunge wa jimbo la Namtumbo Vita Kawawa kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuhakikisha kuwa Kituo cha Afya cha Magazine kinapatiwa gari la kubebea wagonjwa na si vinginevyo.
Mganga Mkuu wa Wilaya Dk. Aron Hyela alisema kuwa Kituo cha Afya cha Magazini kati ya vituo 60 vya kutolea huduma za afya ambacho kipo umbali wa kilomita 230 kutoka makao makuu ya Halamashauri ya Wilaya ya Namtumbo.

Dk. Hyera alisema kuwa kituo cha afya cha Magazini kilipokea zaidi y ash. Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa majengo 5 ambayo ni jengo la Wagonjwa wa nje, upasuaji, maabara, nyumba moja ya mtumishi, jengo la wazazi na chumba cha kuhifadhia maiti ambapo kituo hicho kina jumla ya watumishi 7 sawa na asilimia 13 kati ya 53 ya watumishi wanaohitajika kwa ngazi ya kituo cha afya na kina uwezo wa kuhudumia jumla ya watu elfu 13.
‘’Kituo cha Afya cha Magazini kimepokea sh. milioni 150 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na vifaa vyote vimepokelewa” alisema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Jonah Katanga alisema kuwa halmashauri imetekereza miradi mbalimbali katika kata ya Magazini ikiwemo ujenzi wa kituo cha walimu, nyumba za walimu na miradi mingine ya maendeleo yenye lengo la kuboresha huduma za wananchi.

Naye Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa amewaomba watumishi wa Kituo cha Afya cha Magazini kuona umuhimu wa kulitunza gari la kubebea wagonjwa ambalo litaweza kuwasaidia wakazi Kata ya Magazine pale wanapohitaji kwenda hospitali kubwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi na akina amama wajawazito wanaopata rufaa kwenda hospitali kubwa kwa ajili ya kujifungua.
Aidha amewataka kutotumia gari hilo kwa manufaa yao binafsi ikiwemo kubebea mafuta,babiria na bidhaa zingine na kuwaomba wananchi wa kata hiyo kuendelea kumuunga mkono Rais Samia na Serikali yake kutokana na juhudi mbalimbali anazofanya za kuwaletea maendeleo ikiwemo kuboresha miundombinu kwenye sekta ya afya .