Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WAZIRI wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Masauni ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuuthamini, kuuenzi, kuulinda na kuudumisha Muungano kwa lengo la kusukuma mbele maendeleo ya kiuchumi, kijamii, na kisiasa kwa faida za pande zote mbili za Muungano.

Masauni ameyasema hayo leo Aprili 22, 2025 wakati akifungua kongamano la miaka 61 ya Muungano lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Auditorium Millennium Towers Makumbusho, Dar es Salaam.

Amesema kuwa Muungano umezinufaisha pande zote mbili, hivyo unapaswa kuheshimiwa na kuenziwa milele kwa maslahi ya kila pande.

“Muungano huu ni nguzo imara katika muktadha mzima wa nyanja za maisha yetu kwa kuwa umetufanya kuwa wamoja, kushirikiana, kushikamana na ni msingi wa amani na utulivu, maendeleo na mtangamano wetu na kwamba ndio unaotuimarisha
Ili kuhakikisha kuwa Muungano wetu hautetereki.

“Watanzania hatuna budi kuwaenzi waasisi wa Muungano waliotuachia urithi huu, kwa kuulinda na kuudumisha kwa vitendo kwa kuwa ni nguzo na fahari pekee na ya aina yake katika Bara la Afrika,” amesema Masauni.

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuulinda Muungano na kuyafanyia kazi yake yote yaliyokuwa yanaonekana kama changamoto katika utekelezaji wa masuala yanayohusu Muungano.

“Mpaka zimebaki changamoto tatu tu za kimuungano na ziko kwenye hatua ya utatuzi. Tunamshukuru sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwani tangu aingie madarakani changamoto 15 za kimuungano zimepatiwa ufumbuzi,” amesema.

Hata hivyo Masauni amesema kuna umuhimu wa kutolewa elimu ya Muungano kwa kuwa bado Watanzania wengi wakiwemo vijana hawana uelewa kuhusu masuala na faida zake.

“Kuna haja ya kutolewa kwa elimu ya Muungano kwa makundi mbalimbali ya kijamii na nimefurahi sana kuona vijana wa sekondari na vyuo wakishiriki katika kongamano hili kuwakilisha wenzao”. amesema Waziri Masauni
“Kuna haja ya kutolewa kwa elimu ya Muungano kwa makundi mbalimbali ya kijamii na nimefurahi sana kuona vijana wa sekondari na vyuo wakishiriki katika kongamano hili kuwakilisha wenzao,” amesema Waziri Masauni

Akichangia mada katika kongamano hilo, Waziri na Mbunge mstaafu, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema Watanzania wanapaswa kujivunia Muungano kwa kuwa ulifanyika kwa nchi mbili zilizokuwa changa kuungana pamoja bila ya msaada wa fedha na utaalamu kutoka nchi za kikoloni.

“Muungano huu ulifanikishwa na nchi mbili changa za Afrika bila ya msaada wa fedha na utaalamu kutoka kwa wazungu waliotutawala, tumeingia kwenye Muungano Tanganyika ikiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi minne na siku saba kama Taifa huru lenye mamlaka ndani na nje ya nchi, huku Zanzibar ikiwa na umri wa miezi mitatu na nusu”, amesema Dkt. Mwakyembe

Amewataka wasomi kutoka vyuo vikuu kufanya tafiti zaidi katika historia ya Muungano ili kuweza kupata maarifa ya jitihada zilizofanyika kuwezesha Muungano.