Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma

Mfumo wa eMrejesho toleo la pili (eMrejeshoV2) kutoka Tanzania, umechaguliwa kuwania Tuzo za Mkutano wa Dunia kuhusu Jamii ya TEHAMA mwaka 2025 (World Summit on the Information Society -WSIS 2025).

Tuzo hizi hutolewa chini ya Mkutano wa Dunia kuhusu Jamii ya TEHAMA (World Summit on the Information Society -WSIS), unaoratibiwa na Shirika la Mawasiliano la Umoja wa Mataifa (International Telecommunications Union – ITU), kwa lengo la kutambua na kuchochea miradi bunifu, inayotumia TEHAMA katika kuchangia maendeleo endelevu duniani.

Kwa mujibu wa Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Subira Kaswaga mfumo wa eMrejesho toleo la pili (V2), umechaguliwa katika kipengele cha Serikali Mtandao (e-Government AL C7), ikiwa ni miongoni mwa mifumo 360 ya TEHAMA iliyofuzu hatua ya mchujo kutoka kwa zaidi ya maombi 1000 ya mifumo ya kidijitali yaliyowasilishwa kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Ikumbukwe kwamba, mfumo wa e-Mrejesho toleo la kwanza ulishinda tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Ubunifu katika Huduma za Umma kwa mwaka 2024 ‘UN Public Service Innovation Awards’ .

Amesema, e-GA ilipokea taarifa ya ushiriki wa tuzo hizo hivi karibuni kupitia baruapepe kutoka ITU, baada ya mfumo wa e-Mrejesho kuchaguliwa kuwania tuzo hizo.

Amebainisha kuwa, mfumo wa eMrejesho toleo la pili (V2) ni toleo lililoboreshwa la jukwaa la kidigitali linalotumia akili mnemba (AI) kukusanya, kuchambua, na kutoa mrejesho wa haraka kwa wananchi kuhusu huduma wanazozipokea kutoka taasisi za Serikali na mashirika ya Umma.

“Kupitia jukwaa hili, wananchi wanapata fursa ya kutoa maoni, kupendekeza maboresho, au kueleza changamoto wanazokutana nazo katika kupata huduma na yote haya hutafsiriwa kwa haraka na kwa ufanisi kupitia mifumo ya akili mnemba”, alisema Subira.

Amebainisha kuwa, katika hatua hii ya ushindani kura za umma ndizo zitakazoamua mshindi na kutoa wito kwa Watanzania na wadau wote wa maendeleo ya TEHAMA ulimwenguni, kuunga mkono juhudi za e-GA kwa kupiga kura kabla ya tarehe 30 April, mwaka huu.

“Ni wakati wa kuonyesha mshikamano wetu kama taifa na kanda ya Afrika kwa ujumla, kupitia kura yako, utaiwezesha eMrejesho V2 kuwa mshindi na kushuhudia ubunifu wetu katika TEHAMA unavyoweza kuidhirishia dunia uwezo tulionao”. Amesisitiza Bi. Subira.

Amebainisha kuwa, Washindi wa Tuzo hizo watatangazwa katika Hafla ya Tuzo za WSIS 2025 itakayofanyika wakati wa Tukio la Ngazi ya Juu la Jukwaa la WSIS+20 (WSIS+20 Forum High-Level Event), litakalofanyika mjini Geneva kuanzia tarehe 7 hadi 11 Julai mwaka huu.

Aidha, Subira amesema kuwa, tuzo za WSIS, ni moja ya tuzo za kimataifa zenye heshima kubwa katika uwanja wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hivyo, kuteuliwa kwa e-Mrejesho V2 kuwania tuzo hizo ni heshima kubwa kwa Tanzania.

Mfumo wa e-Mrejesho umesanifiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) na kusimamiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Ili kupiga kura tembelea tovuti ya WSIS Prizes 2025 (https://www.itu.int/net4/wsis/stocktaking/Prizes/2025), tafuta AI Powered eMrejesho V2 kwenye kipengele cha e-Government (AL C7), na piga kura yako sasa ili tulete ushindi nyumbani. #WSIS.