Chuo kikuu cha Harvard kimeushitaki utawala wa rais wa Marekani Donald Trump kutaka kuzuia ufadhili kutoka kwa serikali ya shirikisho.
Chuo kikuu cha Harvard nchini Marekani kimeushitaki utawala wa rais Donald Trump katika mahakama ya shirikisho jana Jumatatu katika juhudi ya kuzuia kufungiwa mabilioni ya dola kama ufadhili wa serikali ya shirikisho.
Hayo ni kwa mujibu wa rais wa chuo hicho Alan Garber. Garber amesema wamewasilisha shauri mahakamani kwa sababu hatua ya utawala wa Trump ni kinyume na sheria na inachupa mipaka ya mamlaka ya serikali.
Kesi hiyo iliyowasilishwa katika mahakama ya Massachusetts, inawalenga maafisa kutoka wizara ya afya na huduma kwa umma, wizara ya sheria, elimu na ulinzi, pamoja na nyingine.
Kwa mujibu wa jarida la Wall Street kesi hiyo inakuja baada ya utawala wa Trumo kutishia kuzuia dola bilioni moja zaidi kama ufadhili wa serikali ya shirikisho, kufuatia hatua ya awali ya kuzuia dola bilioni 2.2.
