Na Mwandishi Wetu, JammhuriMedia, Dar es Salaam
Wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania wameisifu Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa maboresho ya miundombinu yanayoendelea katika bandari zake hapa nchini, hatua ambayo wamesema imechangia bidhaa zao kufika sokoni kwa wakati na kuiwezesha serikali kukusanya mapato .
Hatua hii inakuja baada ya TPA kuimarisha na kupanua uwezo wa bandari zake unaofanywa na Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na wawekezaji.
Maboresho hayo, hususan katika Bandari mbalimbali ikiwemo ya Dar es Salaam, yanajumuisha utoaji wa mizigo kwa haraka zaidi, mifumo bora ya usalama, na miundombinu ya kisasa inayowezesha meli kubwa zaidi kushusha mizigo kwa ufanisi mkubwa.
John Mwakibete, mfanyabiashara kutoka Mbeya amesema kuwa hapo awali alilazimika kusubiri hadi wiki mbili ili mzigo wangu utolewe bandarini, lakini hivi sasa inachukua wastani wa siku tano hadi tatu kutoa mzigo huo na kuwafikishia wateja.
“Hii inanisaidia mimi kukua zaidi kibishara na Serikali kupata kodi na kuwatumikia wananchi,” amesema.
Zainabu Kisanga, mfanyabishara wa vifaa vya umeme kutoka Mwanza anaishukuru TPA kwa maboresho hayo akisema kuwa muda ni pesa katika biashara.
“Kadri ninavyopata mzigo mapema, ndivyo ninavyoweza kuusambaza haraka kwenye maduka. Maboresho yaliyofanyika Bandari ya Dar es Salaam yamepunguza ucheleweshaji na kupunguza gharama za uendeshaji,” alisema katika mahojiano.
Mfanyabiashara kutoka Mtwara, Fatuma Athuman, anayejihusisha na biashara ya vifaa vya kilimo, amesema anaitumia zaidi bandari ya Mtwara na kufurahia huduma zinazotolewa kwa sasa.
“Bandari ya Mtwara sasa ni rafiki kwa wafanyabiashara. Hata wakati wa msongamano, huduma zinatolewa kwa ufanisi. Maboresho haya katika bandari zote , hasa katika Bandari ya Dar, yanaiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya ushindani kikanda.”amesema.
Wafanyabiashara wa mipakani pia wameeleza kuridhishwa kwao na maboresho hayo, ambapo Esther Nyirenda, mfanyabiashara wa mipakani kutoka Kigoma anayeshughulika na bidhaa kutoka Zambia amesema ushindani wa biashara unaenda sambamba na huduma nzuri za bandari.
“Kuna uratibu mzuri zaidi sasa. Utoaji wa mizigo ni rahisi na wa haraka. Hii si kwa faida ya Watanzania tu, bali kwa kanda nzima ya Afrika Mashariki,” alisema.
TPA imechukua hatua mbalimbali katika maboresho haya, ikiwemo kupitia Mradi wa Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP) kwa bandari ya Dar es Salaam , ambao ni mpango mkubwa wa kisasa wa kuongeza uwezo na ufanisi wa bandari kupitia maboresho mbalimbali.
Maboresho hayo yanajumuisha kukamilika kwa ujenzi wa
gati namba 1 hadi 7 ambazo sasa zina uwezo wa kuhudumia meli kubwa zenye urefu wa hadi mita 305 na uwezo wa kubeba makontena 8,000.
Kuongezwa kwa eneo la kuhifadhia magari lenye ukubwa wa mita za mraba 73,000, likiwa na uwezo wa kushughulikia magari 280,000 kwa mwaka.
Kuongezwa sehemu ya kugeuzia meli, kutoka mita 12 hadi 15.5 na kupanuliwa kutoka mita 140 hadi 170, hivyo kuruhusu meli kubwa zaidi kushughulikiwa.
Ujenzi wa mtandao wa reli ya kisasa (SGR) ndani ya bandari na usimikaji wa mfumo wa umeme wa uhakika ili kuongeza ufanisi wa kazi bandarini ni sehemu ya maboresho hayo.
Maofisa wa TPA wanasema maboresho haya ni sehemu ya mpango unaendelea katika bandari mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na ujenzi mpya wa Bandari ya Mbamba Bay iliyopo Songea.
Maboresho hayo pia yamepongezwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia ziara zao hivi karibuni.
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC)pamoja na Kamati ya Miundombinu hivi karibuni walitembelea Bandari ya Dar es Salaam na kupongeza matumizi mazuri ya fedha za umma na maendeleo ya mradi huo.
Mwenyekiti wa PAC, Nagy Kaboyoka, alisema “Baada ya kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), tuliamua kuja kuona wenyewe namna fedha za mradi wa DMGP zinavyotumika. Tunaridhika kuwa uwekezaji huu umetekelezwa kama ilivyopangwa.”
Kaboyoka pia aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi ya TPA na Mkurugenzi Mkuu, Bw. Plasduce Mbossa kwa usimamizi bora wa fedha za miradi na uongozi makini katika mabadiliko ya bandari hiyo.
