Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88.
Uongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Vatican kupitia Kadinali Kevin Farell umetangaza siku ya Jumatatu (21.04.2025) kifo cha Papa Francis kupitia televisheni ya Vatican.
Wiki kadhaa zilizopita, Papa Francis ambaye jina lake halisi ni Jorge Mario Bergoglio kutoka Argentina, alilazwa kwa zaidi ya mwezi mmoja katika hospitali ya Gemelli mjini Roma alipokuwa akisumbuliwa na matatizo makubwa ya kupumua.
Viongozi mbalimbali duniani wameanza kutuma salamu za rambirambi kwa kiongozi huyo mkuu wa Kanisa Katoliki ambaye jana Jumapili katika sikukuu ya Pasaka alionekana akiwa dhaifu baada ya kuzongwa na maradhi.
Papa Francis alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki mnamo Machi 13 mwaka 2013.
