Watu saba wamefariki dunia na wengine 15 kujeruhiwa baada ya kutokea ajali ya barabarani iliyohusisha gari la wagonjwa lenye namba za usajili STM 7840 na pikipiki ya magurumu matatu ya kubeba mizigo wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo baada ya kuwatembelea majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Mafinga Mjini hapo jana.

Alisema ajali hiyo ilitokea jana asubuhi katika eneo la Luganga, baada ya bajaji ya mizigo iliyokuwa imebeba watu 22 waliokuwa wakielekea shambani kugongana uso kwa uso na gari la wagonjwa lililokuwa linatokea Luganga.

“Kumetokea ajali katika eneo la Luganga ambayo imepoteza maisha ya watu saba na kujeruhi wengine 15. Taarifa zinaonesha kuwa walikuwa njiani kuelekea shambani walipogongana na gari la wagonjwa,” alisema Dk Salekwa.

Aidha, aliwataka wananchi kuzingatia matumizi ya vyombo rasmi vya usafiri na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha madhara yanayoweza kuepukika.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mafinga Mjini, Dk Victor Msafiri alithibitisha kupokea miili sita ya wanawake pamoja na mwanaume mmoja aliyefariki wakati akipatiwa matibabu.

“Tumepokea pia majeruhi 15, wanaume saba na wanawake wanane,” alisema.

Aliongeza kuwa majeruhi wote wanaendelea vizuri, japokuwa wanne kati yao wanahitaji uangalizi wa karibu.