Kwa mara ya kwanza duniani, China iliandaa nusu-marathon ya roboti zinazofanana na binadamu mjini Beijing siku ya Jumamosi.
Katika tukio hili la kihistoria, roboti na binadamu walikimbia katika njia moja lakini kwa nyuso tofauti, ikiwa ni mara ya kwanza kushuhudiwa kwa aina hii ya mashindano, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya China.
Jumla ya roboti 20 kutoka timu mbalimbali nchini China zilishiriki katika mashindano hayo. Njia ya mashindano yenye urefu wa kilomita 21 ilikuwa na mazingira tofauti tofauti ikiwemo milima midogo na miinuko, badala ya kuwa tambarare tu, hali iliyotoa changamoto kwa uwezo wa roboti katika uhamaji na kunyumbulika.
Ili kuboresha utendaji wao, kila timu ilifanya marekebisho kwenye roboti zao kwa ajili ya kukimbia umbali mrefu.
Kwa mfano, baadhi waliboresha vifaa vya nyayo za roboti ili ziweze kuhimili uvaaji kwa muda mrefu, huku wengine wakibadilisha namna ya kutembea na mwendo wa roboti kupitia algoriti kwa lengo la kuongeza muda wa matumizi ya betri.
Kwa mujibu wa waandaaji, tukio hilo halikuwa tu mashindano ya michezo, bali pia ni jaribio la uwezo wa jumla wa roboti hizo za ‘humanoid’, ikiwa ni pamoja na kutegemewa, uimara na usalama.
Vituo nane vya “vinywaji” kwa ajili ya roboti pia vilitayarishwa, ambapo roboti ziliweza kubadilishiwa betri. Mwisho wa mashindano, roboti iitwayo “Tiangong Ultra” iliibuka mshindi kwa kukimbia kwa kasi ya takribani kilomita nane kwa saa.
