Israel haijaondoa uwezekano wa kuvishambulia vituo vya nyuklia vya Iran katika miezi ijayo licha ya Rais Donald Trump kumwambia Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwamba Marekani kwa sasa haiko tayari kuunga mkono hatua kama hiyo, kulingana na afisa mmoja wa Israel na watu wengine wawili wanaofahamu suala hilo.
Maafisa wa Israel wameapa kuizuia Tehran kupata silaha za nyuklia na Netanyahu amesisitiza kuwa mazungumzo yoyote na Iran lazima yaongoze kwenye kuvunjwa kabisa kwa mpango wake wa nyuklia. Wapatanishi wa Marekani na Iran wanatarajiwa kufanya duru ya pili ya mazungumzo ya awali ya nyuklia mjini Rome leo Jumamosi.
Katika miezi iliyopita, Israel imependekeza kwa utawala wa Trump machaguo kadhaa ya kushambulia vituo vya Iran, ikiwa ni pamoja na baadhi ya chaguzi zenye muda uliopangwa mwishoni mwa masika na majira ya joto, vyanzo vilisema.
Mipango hiyo inajumuisha mchanganyiko wa mashambulizi ya anga na operesheni za makomando ambazo zinatofautiana kwa ukali na ukubwa na zinaweza kuchelewesha uwezo wa Tehran wa kutengeneza silaha za nyuklia kwa miezi michache tu au mwaka mmoja au zaidi, vyanzo vilisema.
Gazeti la The New York Times liliripoti Jumatano kwamba Trump alimwambia Netanyahu katika mkutano wa White House mapema mwezi huu kwamba Washington ilitaka kuweka kipaumbele kwenye mazungumzo ya kidiplomasia na Tehran na kwamba hakuwa tayari kuunga mkono shambulio dhidi ya vituo vya nyuklia vya nchi hiyo kwa muda mfupi.
