Zaidi ya watu 70 wameuawa na idadi isiyojulikana kujeruhiwa kufuatia shambulio la anga la Marekani kwenye bandari muhimu ya mafuta inayoshikiliwa na waasi wa Houthi nchini Yemen.
Zaidi ya watu 70 wameuawa na idadi isiyojulikana kujeruhiwa kufuatia shambulio la anga la Marekani kwenye bandari muhimu ya mafuta inayoshikiliwa na waasi wa Houthi nchini Yemen.
Shambulio hilo limeonyesha ongezeko la kampeni ya kijeshi ambayo Rais wa Marekani Donald Trump aliianzisha mwezi uliopita dhidi ya kundi hilo la waasi linaloungwa mkono na Iran.
Shambulio hilo katika bandari ya Ras Isa limesababisha milipuko mikubwa ya moto na kuunguza malori ya mafuta. Lilikuwa ni shambulio la kwanza la Marekani kwenye kituo cha mafuta katika kampeni yake mpya ya kupambana dhidi ya waasi wa Kihouthi.
Shambulio hilo limetokea saa chache kabla ya Marekani kuanza tena mazungumzo na Iran mjini Roma, Italia juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Marekani inawalenga Wahouthi kutokana na hatua yao ya kuzishambulia meli kwenye bahari ya Sham ambayo ni njia muhimu ya biashara ya kimataifa.
Waasi wa kihouthi walitangaza kwamba watazishambulia meli za Israel na Marekani katika bahari hiyo kama sehemu ya kuonyesha uungaji mkono wao kwa Wapalestina wanaokabiliwa na vita katika ukanda wa Gaza.
