Na MwandishinWetu, JamhuriMedia, Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema haitenganishi watoto na familia zao bali watoto wanaotupwa au kutelekezwa Serikali huwachukuwa na kuwalea katika mazingira yanayostahiki ili waweze kupata haki zao za msingi.

Kauli imetolewa mwanzoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Anna Athanas Paul katika kikao kilichofanyika Makao ya Watoto Kurasini jijini Dar es Salaam baina ya Wizara hiyo, Wajumbe wa kamati ya Ustawi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Amesema Serikali imejenga nyumba ya kulea watoto ipo Mazizini lakini haiwatenganishi na familia zao, ila kwa wale Watoto waliotupwa katika mabede ya taka hulelewa Moja Kwa Moja na Serikali kwa sababu hawana wazazi.

Ameeleza Zanzibar hakuna watoto wa mitaani isipokuwa kuna familia zenye Mazingira magumu, ambazo huwatumikisha watoto katika biashara ndogo ndogo za kuuza mayai na vitu mbali mbali lakini Serikali huwa inakomesha vitendo vya kuwatumikisha Watoto.

Hata hivyo Naibu Waziri huyo ametoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kuwatumikisha Watoto wanye umri mdogo kwani baadhi ya watu huwaajri kwaajili ya kazi za nyumbani kupika na kulea Watoto wenzao.

Amesema sio kitendo kizuri kwani kila mtoto aliyechini ya umri wa miaka 18 anahitaji kupata haki zake za msingi ikiwemo elimu, malezi bora, matibabu, nk.

Amefahamisha kwamba watu wanaotaka kuwasili mtoto/Watoto hupatiwa kupitia Wizara hiyo, ili watoto hao wakikuwa waone wana wazazi wao kama wengine.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Abeida Rashid amesema Zanzibar imepata eneo kubwa la kujenga kituo kikubwa cha kuwalea watoto ili waweze kuweka Mazingira mazuri na pamoja na kuingiza stadi za maisha ikiwemo kuwafundisha kilimo na ufugaji wa kuku kama walivyoshuhudia katika Makao ya Watoto kurasini.

Amesema SMZ inawalea watoto 26 katika nyumba ya Mazizini na inawapa huduma zote ikiwemo elimu, afya na malazi pamoja na fedha za matumizi mbali mbali ambazo hutolewa kila mwezi.

kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Sabiha Filfil Thani amehimiza masuala ya usalama na ulinzi kwa watoto yanatakiwa kuimarishwa wakati wote katika kituo.

Aidha amewapongeza wahudumu wa kituo hicho na kuwahimiza waendelee kuwa walezi Bora, na kuwaonyesha upendo watoto, Mungu atawalipa kheri na watoto watawajengea imani kubwa dhidi yao.

Pia amepongeza Serikali chini ya uongozi wake RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuipa asilimia 100 ya bejti kituo hicho ili kiweze kutoa huduma vizuri.

Nae Meneja wa Makao ya Watoto Kurasini Twaha Kibalula amesema Makao ya Watoto Kurasini yalianzishwa mwaka 1966 na Serikali chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa lengo la kutoa huduma kwa watoto walio katika Mazingira hatarishi ikiwemo watoto wenye ulemavu na watoto waliopotezana na familia zao.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2022/2023 hadi 2023/2024 kituo kimehudumia watoto 209 kati yao wavulana 160 na wasichana 49, ambapo katika kati yao watoto 18 ni wenye ulemavu.

Ameeleza kwa sasa kituo kina watoto 82, na kinaendesha miradi mdogo midogo ya uzalishaji Mali kama ufungaji kuku na kilimo cha bustani ya mboga mboga za majani husaidia katika mlo, watoto kujifunza kilimo na ufugaji. Pia husaidia katika kutatua changamoto za matumizi madogo madogo ya fedha yanapojitokeza.

Viongozi wa Wizara ya MJJWW kwa kushirikiana na Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi siku ya tarehe 14/04/2025 wamefanya ziara ya kutembea Makao ya Watoto Kurasini, Dar es Salaam kwa lengo la kubadilishan auzoefu katika utowaji wa huduma kwa Watoto wenye mazingira magumu.

Makao hayo yako chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.